Customer Feedback Centre

Ministry of Health

UMOJA WA MAAFISA WATENDAJI WAKUU TANZANIA (COErt) WAMKUBALI PROF. JANABI KUTOKANA NA UONGOZI WAKE MAHIRI

Posted on: October 22nd, 2023


Umoja wa Maafisa Watendaji Wakuu Tanzania wakiwemo wa mashirika binafsi na Serikali (CEOrt) umempongenza Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), Prof. Mohamed Janabi kutokana na uongozi wake mahiri wa kuiboresha MNH na sekta ya afya kwa ujumla wake.


CEOrt ni Umoja wa Maafisa Watendaji Wakuu Tanzania unaowajumuisha watendaji kutoka mashirika binafsi na Serikali wenye wanachama 200 ambao hukutana mara kwa mara na wadau mbalimbali pamoja na Serikali ili kujadili na kutoa mawazo kwa lengo la kuimarisha maendeleo ya kiuchumi nchini.


Kauli hiyo ya pongezi imetolewa na Mkurugenzi Mtendaji wa CEOrt Bi. Santina Benson wakati akiwasilisha salamu hizo kwa niaba ya Bodi ya taasisi hiyo kwa Prof. Janabi ambaye alikua mzungumzaji mkuu katika kikao cha kawaida cha wajumbe wa umoja huo kilichofanyika mapema wiki hii Jijini Dar es Salaam.


Bi. Santina amesema Prof. Janabi alitoa wasilisho lililoamsha hamasa na kuwataka wajumbe wa CEOrt kutazama upya suala la lishe na kutoa kipaumbele kuhusiana na mtindo bora wa maisha. 


“Wasilisho la Prof. Janabi limetupa funzo na mtazamo mpya wa kuwashirikisha wajumbe wetu na kuona namna ambavyo sekretariati inaweza kutafuta mada mbalimbali muhimu zinazoleta changamoto katika jamii ikiwemo afya na kutafuta ufumbuzi wake ”, amesisitiza Bi. Santina.


Amesema, CEOrt itaendelea kufuatilia utendaji wa Prof. Janabi ili kujifunza na pia kuona namna ya kushirikiana naye ili kutafuta jinsi sekta binafsi inavyoweza kutoa mchango wake katika uboreshaji wa sekta ya afya nchini.


Mapema wiki hii, Klabu ya Rotari Dar es Salaam Mzizima ilimpatia tuzo ya umahiri Prof. Janabi kutokana na utendaji wake na mchango anaoutoa kwenye jamii hususani sekta ya afya ikiwemo kutumia muda wake wa ziada kuelemisha jamii kujikinga na maradhi mbalimbali ikiwemo lishe bora.