Customer Feedback Centre

Ministry of Health

UJIO WA KADI ZA KLINIKI KICHOCHEO CHA UIMARISHAJI WA HUDUMA ZA AFYA YA MJAMZITO NA MTOTO

Posted on: June 25th, 2024

.


Na WAF - KAGERA


Mkoa wa Kagera umekuwa mstari wa mbele kupunguza vifo vya mama na mtoto, hivyo ujio wa kadi za Kliniki za Afya ya Wajawazito na watoto utakuwa kichocheo cha uimarishaji wa huduma katika mkoa huo.


Katibu Tawala wa Mkoa wa Kagera, Bw. Steven Ndaki, ameyasema hayo leo Juni 25, 2024, wakati akipokea vitabu vya Kliniki ya wajawazito na watoto katika ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Kagera.


Amesema Mkoa wa Kagera umepokea vitabu vya Kliniki vya wajawazito na watoto. Jumla ya vitabu 63,473, vikiwemo vitabu 31,411 vya ukuaji wa mtoto na vitabu 31,411 vya wajawazito


"Nashukuru Serikali kwa kuwezesha kutupatia kadi hizi kwa ajili ya wajawazito na watoto. Tulikuwa na changamoto ya upatikanaji wa kadi hizi lakini hii itaenda kutatua changamoto hii kwa muda mrefu," amesema Bw. Ndaki.


Aidha, Bw. Ndaki ametilia mkazo juu ya marufuku uuzwaji wa kadi hizo na kusisitiza watoa huduma za Afya kutumia kadi hizo kama ilivyokusudiwa ili kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma ya afya ya mama na mtoto.


Kwa upande wake, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Dkt. Samwel Laiser, amesema kadi za kliniki zitasambazwa katika halmashauri zote nane za Mkoa wa Kagera na kuwataka viongozi wa afya katika ngazi zote kuhakikisha usambazaji na matumizi ya kadi hizi yanazingatia maadili na taratibu zilizowekwa.


Aidha, Dkt. Laiser amesisitiza umuhimu wa wananchi kuzingatia matumizi sahihi ya kadi hizi ili kuboresha afya za mama na mtoto katika jamii pamoja na kutoa rai kwa wananchi kutoa taarifa endapo wataona kadi za kliniki za wajawazito na watoto zikiuzwa katika vituo vya afya.


“Serikali kupitia Wizara ya Afya imetoa kadi hizi kwa lengo la kufuatia afya ya mama na mtoto hivyo zinatolewa bure katika vituo vya kutolea huduma za afya, hivyo ushirikiano wa jamii ni muhimu katika kuhakikisha kadi hizi zinatumika kama ilivyokusudiwa na Serikali” Amesema Dkt. Laiser 


MWISHO.