Customer Feedback Centre

Ministry of Health

TUZINGATIE KANUNI ZA AFYA KUKABILIANA NA MAGONJWA YA MLIPUKO

Posted on: May 25th, 2023

Na. HPS - MoH

Watanzania wametakiwa kuendelea kuzingatia kanuni za afya ikiwa ni pamoja na kuyaweka mazingira katika hali ya usafi ili kujikinga na Magonjwa ya Mlipuko.

Hayo yamesemwa na Mganga Mkuu Halmashauri ya Wilaya ya Muleba Dkt. Kisaka Deo, baada ya kufanya ziara katika visiwa vya Goziba, Kerebe na Nyaburo vilivyopo ndani ya ziwa Victoria kwa ajili ya kujionea namna Elimu ya Afya ilivyozaa matunda katika kukabiliana na magonjwa ya mlipuko ikiwemo Marburg Mkoani Kagera.

“Ili kujikinga na Magonjwa yote lazima tuyaweke mazingira yetu katika hali ya usafi, unaponawa mikono haujikingi na ugonjwa wa Marburg pekee bali inasaidia kujikinga na magonjwa kama vile kuhara, Kipindupindu na kuumwa tumbo.“ Amesema Dkt. Deo

Aidha, Dkt. Kisaka amewahimiza mama wajawazito kuwa na desturi ya kuwahi kliniki mapema pamoja na kuwapeleka watoto kwenye vituo vya kutolea huduma za afya ili kupata chanjo mbalimbali.

Kwa upande wake Afisa Mtendaji kata ya Kerebe Kanali Sefu amesema serikali imechukua hatua madhubuti katika kukabiliana na magonjwa ya mlipuko.

Nao, baadhi ya wananchi akiwemo mkazi wa kisiwa cha Nyaburo Bi. Mary Josephat ameishukuru Serikali kwa kuondoa hofu na taharuki kwa wananchi kwa utoaji wa Elimu ya Afya hali ambayo imesabibisha kuzingatia kanuni za afya na kuendelea na shughuli za kila siku.

Ikumbukwe kuwa jumla ya Viongozi Watatu na Wahudumu wa Afya Ngazi ya Jamii (CHW) Sita walifikiwa katika kisiwa cha Goziba kwa kupewa elimu ya magonjwa ya mlipuko huku Wananchi 161 na Wanafunzi 124 wa Shule ya Msingi wote kwa pamoja walifikiwa kupatiwa elimu ya kujikinga na magonjwa hayo katika kisiwa cha Kerebe.