Customer Feedback Centre

Ministry of Health

TEKNOLOJIA ZA URUTUBISHAJI VYAKULA KUSAIDIA KUIMARISHA AFUA ZA LISHE.

Posted on: April 4th, 2025

Na WAF - Songea, Ruvuma

Serikali kupitia Wizara ya Afya imeendelea kuwekeza katika teknolojia za urutubishaji vyakula kwa lengo la kuimarisha afua za lishe (food fortification) ili kukabiliana na upungufu wa madini na vitamini kwa jamii.

Hayo yamesemwa April 3, 2025 mkoani Ruvuma na Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara Mhe. Exaud Kigahe alipokuwa akimuwakilisha Waziri wa Wizara hiyo Mhe. Suleiman Jaffo katika uzinduzi wa kanuni za uongezaji virutubishi kwenye vyakula za mwaka 2024.

Mhe. Kigahe amesema hatua hiyo inalenga kuwawezesha wazalishaji kuongeza virutubishi kwenye unga wa mahindi kwa urahisi na kwa gharama nafuu ikiwa njia mojawapo ya kuhakikisha wananchi wanapata bidhaa bora zenye virutubishi na kwa bei nafuu kwa afya zao.

Amesema Serikali kupitia Wizara ya Afya inatumia teknolojia za kuimarisha afua (food fortification) kwa lengo la kupunguza upungufu wa madini na vitamini kwa jamii, hivyo jamii izijali na kuzitunza kuiwezesha Serikali kulifikia lengo ililojiwekea.

Kuhusiana na kanuni mpya za uongezaji virutubishi kwenye chakula ambazo zimezinduliwa leo amewaelekeza TBS kutoa elimu kwa wadau wote wanaosimamiwa na kanuni hizi wakiwemo wazalishaji wa chakula nchi nzima na kupitia upya viwango ili viendane na
matakwa ya kanuni hizi.

“Napenda kutamka kuwa Wizara inatoa miezi saba (7) kuanzia leo utekelezaji wa kanuni hizi uanze kutekelezwa namaanisha mpaka ifikapo mwishoni mwa mwezi Novemba, 2025, tunatambua baadhi ya wasindikaji wana mikataba ya
kibiashara kwa mfano kwenye kuzalisha vifungashio,” amesema.

Kwa upande wake Mwakilishi wa Waziri wa Afya, Mkurugenzi wa Mafunzo wa Wizara ya Afya, Dkt. Saitore Laizer amesema Serikali inaendelea kushirikiana na wadau kupanua wigo wa urutubishaji na kuzindua mpango wa kitaifa wa kurutubisha chakula kwa kutumia madini chuma, Zinki, vitamini B12 na folic ya asidi kwa unga wa ngano, mahindi na vitamini A kwa mafuta ya kula.