Customer Feedback Centre

Ministry of Health

TANZANIA YAWASILI GENEVA, KUSHIRIKI MKUTANO WA 78 WA SHIRIKA LA AFYA DUNIANI (WHO)

Posted on: May 16th, 2025

Na WAF, Geneva - Uswiz


Ujumbe wa Tanzania, ukiongozwa na Waziri wa Afya wa Tanzania Bara, Mhe. Jenista Mhagama, pamoja na Waziri wa Afya wa Zanzibar, Mhe. Nassor Mazrui, umewasili jijini Geneva, Uswisi, kwa ajili ya kushiriki Mkutano wa 78 wa Shirika la Afya Duniani (WHO) unaotarajiwa kufanyika kuanzia tarehe 19 hadi 27 Mei, 2025.


Ujio wa viongozi hao umepata mapokezi rasmi kutoka kwa Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Ofisi za Umoja wa Mataifa jijini Geneva, Mhe. Balozi Abdallah Possi  Mei 16, 2025.


Kabla ya kuanza kwa mkutano mkuu, kutafanyika Mkutano Maalum wa Kanda ya Afrika utakaofanyika Mei 18, 2025, ukiwa na ajenda mahsusi ya uchaguzi wa Mkurugenzi wa WHO Kanda ya Afrika ambapoTanzania imemsimamisha Prof. Mohammed Janabi, kuwania nafasi hiyo.


Mara baada ya kuwasili, ujumbe wa Tanzania umefanya kikao maalum cha maandalizi ya ushiriki wa nchi katika uchaguzi huo na kuongozwa na Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi kutoka Tanzania, Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, ambaye ameshiriki kwa njia ya mtandao.



Viongozi waliohudhuria kikao hicho ni pamoja na Mhe. Angellah Kairuki, Mhe. Neema Lugangira (Mbunge), Mhe. Balozi Hoyce Temu (Naibu Mkuu wa Ubalozi wa Tanzania, Geneva), Balozi Noel Kaganda, Dkt. Seif Shekalaghe (Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya), Dkt. Grace Magembe (Mganga Mkuu wa Serikali), pamoja na wataalamu kutoka wizara za kisekta za Tanzania