Customer Feedback Centre

Ministry of Health

TANZANIA YAPIGA HATUA KATIKA KUKABILIANA NA MAJANGA NA DHARURA ZA KIAFYA

Posted on: August 19th, 2023

Na WAF – DSM

Serikali ya Tanzania imeonekana kupiga hatua katika kukabiliana na dharura za kiafya pamoja na magonjwa ya milipuko kutoka asilimia 48 mwaka 2016 hadi kufikia asilimia 63 mwaka 2023 mara baada ya kufanyiwa tathmini na wakaguzi kutoka nje ya nchi.

Hayo yamesemwa leo na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Dkt. Grace Magembe wakati akifunga kikao kazi cha tathmini jumuishi ya kupima uwezo wa nchi katika kukabiliana dhidi ya majanga na matukio yenye athari za kiafya kilichofanyika kwa siku tano jijini Dar Es Salaam.

Dkt. Magembe amesema, tathmini iliyofanyika imeangalia utayari wa nchi katika kuzuia, kugundua na kukabiliana na magonjwa ya dharura yanayotishia usalama wa Dunia.

“Baada ya kupata asilimia 48 mwaka 2016 kama nchi tuliamua tujipange upya ili tuweze kufanya vizuri katika tathmini inayofuata ambapo tuliimarisha utayari wa mifumo yetu ya kushughulikia majanga kuanzia ngazi ya jamii hadi vituo vya afya, pia tathmini hii inaangalia Sekta nyingine kama vile chakula, mifugo, kilimo, uvuvi na nyinginezo”. Amesema Dkt. Magembe.

Aidha, Dkt. Magembe ameongeza kuwa, tathmini hiyo iligusa majanga ya athari za kemikali ambapo wakaguzi kutoka nje walikagua kazi za Mkemia Mkuu wa Serikali na Sekta zote mtambuka kwa kushirikiana na Wizara ya Afya kuwa zimejiandaa namna gani kukabiliana dhidi ya majanga na milipuko.

Akitolea mfano mlipuko wa ugonjwa wa Maburg uliotokea mapema mwaka huu Mkoani Kagera, Dkt. Magembe amesema kama nchi ingekua haijajiandaa vizuri kukabiliana dhidi ya milipuko, ugonjwa huo ungeweza kusambaa maeneo mengi zaidi na kuleta athari kubwa.

Kikao hicho kilichojumuisha wakaguzi kutoka nje ya nchi, wajumbe kutoka Sekta mbalimbali nchini na Taasisi za Kimataifa kiliitimishwa na azimio la Tanzania kuendelea kujidhatiti katika kukabiliana dhidi ya athari za kiafya na majanga ili kwenye ukaguzi utakaofuata nchi ikutwe imejiandaa vizuri zaidi ya sasa.