TANZANIA, WADAU KUWEKA KIPAUMBELE USALAMA WA MGONJWA
Posted on: April 5th, 2025
Na WAF - Manila, Ufilipino
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeuhakikishia Mkutano wa Saba (7) wa Mawaziri wa Afya ulimwenguni kuwa itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali katika kuhakikisha usalama wa mgonjwa unapewa kipaumbele kwakuwa suala hilo ni mtambuka.
Mkurugenzi wa Tiba Wizara ya Afya Dkt. Hamad Nyembea amesema hayo leo Aprili 4, 2025 akimwakilisha Waziri wa Afya Mhe. Jenista Mhagama kwenye Mkutano wa Saba (7) wa Mawaziri wa Afya ulimwenguni unaofanyika katika mji wa Manila nchini Ufilipino, unaolenga kujadili usalama wa mgonjwa.
"Tanzania ina mikakati mbalimbali ya kuhakikikisha usalama wa mgonjwa unapewa kipaumbele ikiwa ni pamoja na uwepo wa miongozo na sera tuliyojiwekea katika ngazi mbalimbali, utumiaji wa nyezo mbalimbali zilizotolewa na Shirika la Afya Duniani (WHO) na kutoholewa nchini," amesema Dkt. Nyembea.
Amesema, mikakati mengine inayochukuliwa na Tanzania katika kuhakikisha usalama wa mgonjwa ni kusaidia usimamizi wa usalama wa mgonjwa pamoja na uwepo wa mifumo ya ufuatiliaji wa usalama wa mgonjwa.
Aidha, Tanzania ni miongoni mwa nchi 27 zilizoshiriki katika mkutano huo sambamba na nchi za Estawini, Micronesia, Gambia, Jamaica, Maldives, Papua New Guinea, Tajikistan, Tuvalu, Angola, Cambodia, Chinese Taipei, Fiji, Georgia, Ujerumani, Indonesia, Japan, Kenya, Libya, Mongolia, Panama, Russia, Slovakia, Sudan Kusini, Timot Leste, Zimbabwe pamoja na Uingereza (UK).
Kauli mbiu ya Mkutano huo ni "kuwekeza nguvu katika mustakabali wa usalama wa mgonjwa katika utoaji wa huduma za usalama wa Afya ya Mgonjwa."