Customer Feedback Centre

Ministry of Health

TANZANIA, SOMALIA ZATIA SAINI USHIRIKIANO SEKTA YA AFYA

Posted on: December 20th, 2024

Na WAF-Mogadishu, Somalia

Naibu Waziri wa Afya, Dkt. Godwin Mollel ameshiriki hafla ya utiaji saini Makubaliano ya Ushirikiano na Hati za Makubaliano (MoU) kati ya Serikali ya Somalia na Tanzania katika sekta ya Afya yanayolenga katika maeneo muhimu ambayo yataimarisha ustawi wa afya za wananchi wa nchi zote mbili.

Dkt. Mollel amesaini makubaliano hayo kwa niaba ya Waziri wa Afya Mhe. Jenista Mhagama mapema leo tarehe 19 Desemba 2024 Jijini Mogadishu akiyataja maeneo muhimu yatakayopewa vipaumbele katika Afya.

Maeneo muhimu yatakayowekewa mkazo ni ubingwa na ubingwa bobezi, ubadilishanaji rasilimali watu kwa sekta kwa nchi hizi mbili na kuwajengea uwezo watumishi wa afya.

Maeneo mengine muhimu ni tafiti na ubunifu, upatikanaji wa bidhaa za afya, na huduma za afya mtandao (Digital Health).

Msisitizo pia utawekwa katika tiba utalii, kubadilishana uzoefu na usimamizi wa mnyororo wa ugavi wa bidhaa za afya, sambamba na kutafuta rasilimali kwa ajili ya kuboresha huduma za afya.

Ujumbe wa Tanzania uliongozwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Mohammed Thabit Kombo, huku Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Balozi Dkt. Pindi Chana, pia akiambatana nao katika tukio hili muhimu.

Makubaliano haya yanatarajiwa kukuza uhusiano wa kidiplomasia kati ya Tanzania na Somalia.