TANZANIA, KOREA KUSINI KUSHIRIKIANA KUENDELEZA TIBA ASILI
Posted on: August 20th, 2025
Na, WAF-Seoul, Korea Kusini
Serikali ya Tanzania imeanza hatua za kuimarisha ushirikiano na Korea Kusini katika nyanja za ubunifu, uhamishaji wa teknolojia na uendelezaji wa bidhaa za tiba asili.
Hayo yamebainika Agosti 19, 2025 Jamhuri ya Korea Kusini, wakati wa ziara ya Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa (NIMR), Prof. Said Aboud, pamoja na Kaimu Mkurugenzi Msaidizi wa Tiba Asili kutoka Wizara ya Afya, Dkt. Winifrida Kidima, ambao wamefanya ziara ya heshima katika Ubalozi wa Tanzania nchini Korea Kusini na kukutana na Balozi wa Tanzania nchini homo, Mhe. Togolani Mavura.
Katika mazungumzo yao, viongozi hao wamejadili maendeleo ya sekta ya tiba asili nchini Korea na fursa za kubadilishana uzoefu ambazo zitasaidia kuongeza uwezo wa Tanzania katika nyanja mbalimbali ikiwemo ubunifu, uendelezaji wa bidhaa, biashara ya tiba asili, uanzishaji wa makampuni changa (startups), na tafiti za majaribio ya kitabibu (clinical trials).
Aidha, mazungumzo hayo yamehusisha pia ushirikiano katika uzalishaji wa viambato hai vya dawa (API) na utungaji wa sera.
Prof. Aboud amesisitiza umuhimu wa kujenga uwezo kwa watafiti na wadau wa tiba asili nchini, akieleza kuwa Tanzania ina fursa kubwa kupitia mimea dawa ambayo inahitaji utafiti wa kitaalam ili kuhakikisha usalama, ufanisi na ubora.
Kwa upande wake, Dkt. Kidima amebainisha kuwa Tanzania imeweka mazingira wezeshi ya huduma za tiba asili, ambapo huduma hizo tayari zimeanza kutolewa katika Hospitali za Rufaa na za Kanda 14 nchini.
Aidha amesisitiza kwamba uzoefu wa Korea unaweza kusaidia kuboresha zaidi utoaji wa huduma hizo na kuongeza uwezo wa wataalam wa afya nchini.