Customer Feedback Centre

Ministry of Health

TANZANIA INATUMIA SHILINGI LAKI NNE KWA KILA MWENYE VVU

Posted on: December 2nd, 2024

Na WAF - Ruvuma

Waziri wa Afya Mhe. Jenista Mhagama amesema Serikali inatumia shilingi 400,000 kwa Mtanzania mwenye maambukizi ya Virusi Vya Ukimwi (VVU) kila mwaka ikiwa ni sawa na Shilingi bilioni 750 kwa WAVIU milioni 1.7 waliopo nchini.

Waziri Jenista amesema hayo leo Jumapili, Desemba Mosi, 2024 kwenye kilele cha maadhimisho ya Siku ya UKIMWI Duniani ambayo kitaifa yanaadhimishwa mjini Songea mkoani Ruvuma, katika viwanja vya Maji Maji huku Makamu wa Rais, Dk Isdory Mpango akiwa mgeni rasmi.

"Inakadiriwa kila mwaka kila mtu anayeishi na VVU katika Taifa letu anatumia fedha zisizopungua
Shilingi 400,000 na kama tunavyojua wenye maambukizi ni milioni 1.7 nchini, hivyo tukitumia zaidi ya Shilingi bilioni 750 kila mwaka kuhakikisha tunafubaza VVU na UKIMWI ndani ya Taifa letu," amesema Waziri Jenista.

"Gharama hii ni kubwa, tuna kila sababu kuzuia maambukizi mapya nchini na kuhakikisha walio katika dawa wanafubaza virusi vya kwa kutoa tiba stahiki na kuhakikisha WAVIU wote wanaendelea kufubaza VVU na wataendelea kulindwa katika uhai wao," ameongeza Waziri Jenista.

Aidha, Waziri Jenista ametoa wito kwa jamii kuepuka tabia ambazo zinatajwa kuwa viashiria na chanzo cha maambukizi mapya ikiwemo unywaji wa pombe kupindukia, kuwa na wapenzi wengi pamoja na ngono zembe.