TANZANIA HAINA UGONJWA WA MARBURG TUMEUDHIBITI
Posted on: March 13th, 2025
Na WAF - Biharamulo, Kagera
Waziri wa Afya Mhe. Jenista Mhagama amesema Tanzania imefanikiwa kuudhibiti ugonjwa wa mlipuko wa Marburg na ameutangazia Umma wa Watanzania kuwa ugonjwa huo umeisha kutokana na kutokuwepo kwa mgonjwa mwengine yeyote tangu mgonjwa wa mwisho alipopatikana tarehe 28 Januari, 2025 na hadi kufikia tarehe 11 Machi, 2025 siku 42 zimepita.
Waziri Mhagama amethibitisha hayo leo Machi 13, 2025 alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari wilayani Biharamulo, Kagera kwamba siku 42 zimepita tangu mgonjwa wa mwisho alipofariki mgonjwa wa mwisho afariki na kisayansi Tanzania inakidhi vigezo vya kutangaza kuwa mlipuko huo umeisha.
"Tarehe 20 Januari, 2025, Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, aliutangazia umma na jamii ya Kimataifa juu ya uwepo wa mlipuko wa ugonjwa wa Marburg uliotokea katika wilaya ya Biharamulo mkoani Kagera, naomba nichukue fursa hii leo tarehe 13 Machi, 2025 naomba kumshukuru Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutuwezesha hadi leo hii nautangazia umma na jamii ya Kimataifa kuwa, sasa Tanzania haina mlipuko wa ugonjwa wa Marburg," amesema Waziri Mhagama.
Aidha, Waziri Mhagama ameendelea kuwakumbusha Watanzania juu ya kuchukua tahadhari kwakuwa nchi zinazotuzunguka zinaendelea kukabiliana na magonjwa ya mlipuko ikiwemo Mpox na Ebola, hivyo nchi yetu pia ipo kwenye hatari kutokana na mwingiliano wa shughuli za kijamii na kiuchumi, pamoja na uwepo wa mipaka ya moja kwa moja baina ya nchi hizi.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Kagera Mhe. Hajat Fatma Mwassa ametoa shukran kwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye amekuwa akielekeza na kutoa ushauri wa jinsi ya kudhibiti ugonjwa wa Marbug pamoja na Waziri wa Afya Mhe. Jenista Mhagama aliyekuwa msimamizi wa utekelezaji wa maelekezo ya Rais na hatimaye kuumaliza ugonjwa huu.
Naye, Mganga Mkuu wa Serikali Dkt. Grace Magembe amesema kuwa Serikali imeimarisha miundombinu mbalimbali ili kukabiliana na magonjwa ya mlipuko ikiwemo uimarishaji wa maabara zenye uwezo wa kupima magonjwa ya mlipuko hasa za Taifa, utolewaji wa elimu ya afya kwa umma hasa katika mikoa inayopakana na nchi jirani pamoja na upatikanaji wa huduma za maji safi na salama.