TAASISI YA OCEAN ROAD KUWA KITOVU CHA TIBA UTALII AFRIKA- DKT. MSEMO
Posted on: September 11th, 2025
Na WAF, Dar es Salaam
Uongozi wa Taasisi ya Saratani Ocean Road umesema kuwa umejipanga kuwa kitovu cha Tiba Utalii Afrika, na katika kufanikisha hilo umekutana na wadau wa sekta binafsi kutoka Global Medicare kujadili namna ya kushirikiana ili kufikia lengo hilo.
Akizungumza katika kikao hicho Septemba 11, 2025 Jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi Mkuu wa Global Medicare ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Taifa ya Tiba Utalii, Bw. Abdulmalick Mollel, amesema kuwa tiba utalii ni suala mtambuka linalohitaji ushirikiano mpana ili kufanikisha.
Bw. Mollel amesisitiza kuwa Taasisi ya Saratani Ocean Road ina vigezo vyote vya kuwa kitovu cha tiba utalii kutokana na kuwa na wigo mpana wa wataalam, miundombinu na teknolojia ya uchunguzi na matibabu ya saratani, si kwa Tanzania pekee bali pia kwa nchi jirani, hivyo ni muhimu kuboresha utoaji huduma, kuleta ubunifu katika huduma, na kutangaza huduma hizo ndani na nje ya nchi.
Bw. Mollel pia amempongeza Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi hiyo, Dkt. Diwani Msemo, kwa kasi yake ya utekelezaji na maboresho makubwa ya miundombinu na huduma, ambayo yamepewa kipaumbele katika Mpango Mkakati wa 2025–2030, ambapo Taasisi inalenga kupata ithibati za kimataifa kwa huduma zake za vipimo na matibabu.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Saratani Ocean Road, Dkt. Diwani Msemo, amemshukuru Bw. Mollel kwa utayari wake wa kushirikiana na Taasisi katika kuandaa mpango mkakati wa tiba utalii ambao utaongeza idadi ya wagonjwa kutoka nje.
"Katika mwaka 2024, zaidi ya wagonjwa 384 kutoka Zambia, Malawi, Comoro, Kenya, Msumbiji na Burundi walipata huduma katika Taasisi ya Ocean Road, "amefafanua Dkt. Msemo.
Dkt. Msemo amesema Mpango Mkakati unaoandaliwa unalenga kuitikia wito wa Rais Samia Suluhu Hassan wa kuimarisha tiba utalii nchini.
Dkt. Msemo amesisitiza kuwa menejimenti na wafanyakazi wa Taasisi wanapaswa kuwa tayari kubadili mitazamo yao, kujifunza, na kushirikiana na wenzao wenye uzoefu kutoka sekta binafsi na Serikali katika tiba utalii.
Ajenda ya kukuza tiba utalii nchini Tanzania imeanzishwa na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan na ni miongoni mwa vipaumbele vya Taasisi ya Ocean Road.
Naye Mratibu wa Tiba Utalii Wizara ya Afya Dkt.Asha Mahita amewashukuru wadau kutoka sekta binafsi kwa kuonyesha nia ya kushirikiana na Serikali katika kuhakikisha kuwa Tanzania inafikia lengo la kuwa Kitivo cha Tiba Utalii barani Afrika.