SERIKALI YAPIGA HATUA KUPUNGUZA VIFO VINAVYOWEZA KUZUILIKA VYA MAMA NA WATOTO
Posted on: August 11th, 2026Na Shaban Juma, WAF - Dodoma
Naibu Waziri wa Afya, Dkt. Florence Samizi, kwa niaba ya Waziri wa Afya, Mhe. Mohamed Mchengerwa, amesema Serikali imeendelea kuchukua hatua madhubuti za kuimarisha huduma za afya ya uzazi, mama na mtoto, kwa lengo la kupunguza na hatimaye kukomesha vifo vinavyoweza kuzuilika vya mama wajawazito na watoto wachanga nchini.
Dkt. Samizi ameyasema hayo leo, Agosti 11, 2026, wakati akiwasilisha taarifa ya Wizara ya Afya mbele ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya na Masuala ya UKIMWI kuhusu hali ya vifo vya mama wajawazito na watoto wachanga pamoja na mikakati ya Serikali ya kukabiliana na changamoto hiyo.
Amesema Serikali inaendelea kuweka nguvu katika kuhakikisha mama mjamzito anapata huduma bora na kwa wakati kuanzia kipindi cha ujauzito, wakati wa kujifungua na baada ya kujifungua, huku huduma kwa watoto wachanga zikiendelea kupewa kipaumbele ili kuzuia vifo vinavyoweza kuzuilika.
Dkt. Samizi amesema hatua zinazochukuliwa na Serikali zinahusisha kuimarisha miundombinu ya huduma za afya ya uzazi na watoto wachanga, kuongeza vituo vyenye uwezo wa kutoa huduma za dharura za uzazi na mtoto, pamoja na kuongeza na kuboresha Wodi Maalum za Watoto Wachanga (NCU) katika hospitali mbalimbali nchini.
Aidha, Dkt. Samizi amesema Serikali imeendelea kuhakikisha upatikanaji wa vifaa tiba muhimu kwa ajili ya huduma za watoto wachanga, hususan watoto wanaozaliwa kabla ya wakati au wenye changamoto za kupumua, sambamba na kuimarisha upatikanaji wa oksijeni na huduma nyingine muhimu za kuokoa maisha.
Amesema, Serikali pia imeendelea kuongeza wataalamu wenye ujuzi katika huduma za afya ya uzazi, mama na mtoto, pamoja na kuwajengea uwezo watoa huduma ili waweze kutambua mapema viashiria vya hatari na kuchukua hatua stahiki kwa wakati.
Katika hatua nyingine, Dkt. Samizi amesema mfumo wa M-MAMA umeendelea kuimarisha huduma ya usafirishaji wa haraka wa wajawazito na watoto wanaohitaji huduma za dharura, hatua inayosaidia kupunguza ucheleweshaji wa kuwafikisha wagonjwa kutoka nyumbani kwenda vituo vya kutolea huduma na kutoka kituo kimoja kwenda kingine.