Customer Feedback Centre

Ministry of Health

SERIKALI YAJIPANGA KUKABILIANA NA CHANGAMOTO ZITOKANAZO NA ONGEZEKO LA IDADI YA WATU

Posted on: February 28th, 2024



Na. WAF - Lindi

Serikali kupitia Wizara ya Afya inaendelea na juhudi za kupunguza changamoto katika Sekta ya Afya zinazoendelea kujitokeza kutokana na ongezeko la idadi ya watu pamoja na kubadilika kwa magonjwa ikiwemo magonjwa ya milipuko.

Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu amesema hayo jana Februari 28, 2024 wakati wa majumuisho ya ziara yake kwa siku ya leo katika Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa kwenye Zahanati ya Nangurukuru akiwa kwenye ziara yake ya kikazi ya siku Tatu katika Mkoni Lindi.

“Changamoto katika Sekta ya Afya ni nyingi na dawa yake ni kuzitatua kwa haraka lakini changamoto nyingine hatuwezi kuzimaliza zote kwa Mwaka Mmoja kwa kuwa idadi ya watu inazidi kuongezeka nchini.” Amesema Waziri Ummy.

Amesema changamoto nyingine zinazotokea ni kutokana na mabadiliko ya tabia nchi, rasilimali fedha lakini kutokana na uongozi imara wa Dkt. Samia Suluhu Hassan Sekta ya Afya imeweza kupunguza changamoto nyingi ikiwemo ya Vifaa na Vitaa Tiba kazi iliyobaki ni kwa watumishi wa Afya katika utendaji wao.

Aidha, Waziri @ummymwalimu ameridhishwa na upatikanaji wa dawa katika Hospitali hiyo ambapo amesema miongoni mwa dawa zote alizouliza zipo ikiwezo dawa za kutuliza maumivu kama Panadol, dawa za kuzuia maambukizi (antibiotic), uwepo wa dawa hizo katika Hospitali, Vituo vya Afya na Zahanati unapunguza malalamiko ya upatikanaji wa dawa kwa wananchi.

Pia, Waziri Ummy amewapongeza watumishi katika Sekta ya Afya wanaofanya vizuri katika utendaji kazi wao na kufuata miongozo, taratibu na kanuni katika utendaji kazi wao

“Katika kazi zetu tuzingatie mambo makubwa Matatu, kwanza weledi (Professionalism), la pili maadili (Ethics) pamoja na kuzingatia viapo vya utumishi katika Sekta ya Afya ambayo ni kuokoa maisha ya Watanzania kadri inavyowezekana.” Amesema Waziri Ummy

Mwisho, Waziri Ummy amemshukuru Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa fedha nyingi kujenga miundombinu katika Hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa pamoja na kuongeza watumishi wa Afya zaidi ya 110 ndani ya Miaka Mitatu na anaendelea kutoa vibali vya kuajiri.