SERIKALI YAJA NA MABORESHO YA HUDUMA ZA AFYA KUPITIA AKILI UNDE
Posted on: September 10th, 2025
Na. WAF, Dodoma
Serikali inaendeleza juhudu zake za kuboresha huduma za afya kwa matumizi ya Akili Unde (IA) kuwekeza kwenye vifaa tiba vya kisasa vinavyosaidia kutoa huduma za haraka na kwa ufanisi kwa wananchi.
Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Mifupa na Ubongo,MOI Balozi Dkt. Mpoki Ulisubisya leo Septemba 10, 2025 wakati wa ufunguzi wa Maonesho ya Kimataifa ya Biashara ya Dawa na Vifaa Tiba, jijini Dar es Salaam.
Dkt. Mpoki amesema vifaa vyote vya sekta ya afya vinavyozalishwa vimechukua sehemu ya Akili Unde na vimeboreshwa namna vinavyofanya kazi ili kumrahisishia kazi mtumiaji wakati wa kuwahudumia wagonjwa wengi kwa muda mfupi.
“Akili unde inapunguza muda wa kumuhudumia mgonjwa na kuongeza ufanisi katika kutoa huduma na zile afua zinazoweza kurudisha afya ya mgonjwa iliyoteteleka, na vifaa vinavyohitajika hutumika,” amesema Dkt. Mpoki.
Amesema Tanzania ni lango la kuelekea nchi za SADC na Jumuhia ya Afrika Mashariki, hivyo Serikali imefungua milango ya uwekezaji wa biashara lakini pia viwanda vya dawa na vifaa tiba kwa wawekezaji wa ndani na nje ya nchi.
‘Mtu yeyote atakayeleta biashara Tanzania atakuwa amepata soko kubwa sana la kuuza nchi za SADC na afrika mashariki na kusini mwa afrika,” amesema Dkt. Mpoki.
"Tunapokutana namna hii tunapata fursa ya kubadilishana mawazo yanayotupelekea kuleta afua zitakazokuwa mahususi kwa ajili ya mahitaji ya nchi zetu kwa sababu vifaa vingi vya sekta ya afya vimebuniwa na kutegenezwa na watu ambao walikuwa wanataka kukidhi mahitaji ya nchi husika," amesema Dkt. Mpoki.
Aidha Dr. Mpoki ameongeza kuwa Serikali inapokutana na watengenezaji inakuwa na nafursa ya kutoa maoni yake kulingana na hali ya watu wake .