Customer Feedback Centre

Ministry of Health

SERIKALI YAENDELEA KUDHIBITI KASI YA MAAMBUKIZI MAPYA YA VVU KWA VIJANA BALEHE.

Posted on: October 24th, 2023

Na WAF - MPWAPWA, DODOMA 


Kufuatia ripoti ya tafiti za Viashiria maambukizi ya VVU nchini, Serikali imesema itahakikisha inapunguza hali ya Maambukizi mapya ya VVU kwa vijana wenye umri wa miaka 15-24 hasa wanaosoma shule za Sekondari hususani wasichana.


Hayo yamesemwa na Mganga Mkuu wa wilaya ya Mpwapwa Dkt. Raheem Hangai Wakati wa jukwaa la Jikubali lililokutanisha shule zote za msingi na Sekondari za wilayani hapo katika uwanja wa Magereza, Oktoba 24, 2023.


Dkt. Hangai amesema tafiti za Viashiria vya maambukizi ya VVU nchini zinaonyesha kuwa asilimia 40 ya hali ya maambukizi mapya ya VVU ni kwa vijana wenye umri wa miaka kati ya 15 na 24 huku wasichana wakiwa hatarini zaidi.


"Katika kila watu 10 wanaopata maambukizi mapya ya VVU wanne ni vijana wa umri wa miaka 15-24 ambapo katika kundi hili asilimia 80 ni wasichana, Hali kadhalika katika tafiti zingine zinaonesha kuwa asilimia 14.3 ya vijana wanaume na asilimia 9.1 ya vijana wanawake wanaanza ngono kabla ya miaka 15 hivyo Serikali itahakikisha inatumia majukwaa mbalimbali ikiwemo hili ili kuwapa dhana ya kujikubali na kushinda vishawishi, kuwa bora na kupunguza kasi ya Maambukizi mapya ya VVU nchini". Amesema Dkt. Hangai.


Kwa upande wake Muwakilishi kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Gerald George ametoa sababu za jukwaa la JIKUBALI kuyalenga makundi ya vijana Balehe hasa wanafunzi. 


"Vijana wengi wenye umri wa miaka 15 -24 hawajui hali zao za maambukizi ukilinganisha na watu wenye umri mkubwa, Hali hii inapelekea vijana hawa kutoanza dawa za ARVs mapema au kutokujua namna ya kukabiliana na vishawishi hasa katika zama hizi za Maendeleo ya sayansi na Teknolojia hivyo kutopunguza kasi ya VVU". Amesema Gerald. 


Nae Eunice Mlekwa kutoka shule ya Sekondari Mpwapwa na Emmanuela Michael kutoka Mazae Sekondari wameushukuru Wizara ya Afya kwa kushirikiana na wadau wake kuwafikishia ujumbe wa jukwaa la jikubali kwa wakati sahihi.