SERIKALI, WABUNGE WATOA MSUKUMO MPYA UIMARISHAJI UFADHILI MAPAMBANO DHIDI YA USUGU WA DAWA
Posted on: December 3rd, 2025Na WAF, Dar es Salaam
Serikali na Wabunge walio mstari wa mbele kwenye kutoa msukumo juu ya uimarishwaji wa afua za kutokomeza Usugu wa Dawa (AMR) wamekubaliana kuanzisha mfumo endelevu wa kufadhili afua za kukabili usugu wa vimelea dhidi ya dawa.
Kikao hicho cha awali kabla ya ufunguzi rasmi kimefanyika Desemba 2, 2025 na kuongozwa na Mfamasia Mkuu wa Serikali Bw. Daudi Masasi kando ya Mkutano Mkuu wa wadau hao kutoka barani Afrika, unaofanyika jijini Dar es Salaam
Katika mazungumzo hayo, pande zote zimebainisha changamoto za ufadhili zinazoathiri utekelezaji wa programu za AMR, zikiwemo maeneo ya utafiti, uchunguzi wa maabara, elimu kwa umma, usimamizi wa matumizi ya dawa pamoja na ufuatiliaji wa mwenendo wa maambukizi sugu.
Msasi amesisitiza kuwa mafanikio ya juhudi za kupambana na AMR yanategemea mfumo madhubuti wa rasilimali fedha utakaowezesha afua kutekelezwa kwa ufanisi na kwa wakati.
Kikao hicho cha pembeni kimeazimia kuandaa mkutano wa kitaifa wa “parliamentary dialogue” utakaowakutanisha wabunge, wataalam wa afya, sekta binafsi na wadau wa maendeleo ili kujadili mbinu bora na za kudumu za kufadhili afua za AMR.
Viongozi hao wamekubaliana kuwa uwekezaji katika mapambano dhidi ya AMR ni hatua muhimu kwa kulinda afya ya wananchi, kupunguza gharama za matibabu, kuimarisha uzalishaji wa taifa na kuhifadhi mafanikio yaliyopatikana katika sekta ya afya.
Kikao hicho kimefungua ukurasa mpya wa ushirikiano kati ya Serikali na Bunge katika kuimarisha mapambano dhidi ya usugu wa dawa nchini.
Akizungumza kwenye kikao hicho Katibu wa umoja huo, Mhe. Christina Mzava, amesema ameona dhamira ya wabunge kutetea kipaumbele cha agenda ya AMR katika mijadala ya sera na bajeti za kitaifa.