Customer Feedback Centre

Ministry of Health

SERIKALI KUIMARISHA VIWANDA VYA NDANI VYA DAWA, VIFAA NA VIFAA TIBA

Posted on: August 7th, 2024

Naibu Waziri wa Afya Dkt. Godwin Mollel, amesema kuwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imedhamiria kuendelea kuboresha huduma za afya kwa kuzalisha vifaa, vifaa tiba, pamoja na dawa ili kukidhi mahitaji ya ndani na kupunguza utegemezi wa bidhaa za nje.


Dkt. Mollel amesema hayo leo Agosti 07, 2024, katika ziara ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya na Masuala ya UKIMWI inayoongozwa na Kaimu Mwenyekiti, Mhe. Christine Mnzava, ambapo walitembelea kiwanda kinachozalisha gloves cha Idogloves kinachomilikiwa na Bohari kuu ya dawa MSD kilichopo Idofi, makambako mkoani Njombe.

"Dhamira ya Serikali katika kuanzisha viwanda vya ndani ni kuboresha huduma za afya pamoja na kupunguza gharama za vifaa nchini. Hii itasaidia pia kuongeza ajira kwa Watanzania, na ndio maana Rais Dkt. Samia amewekeza kwenye sekta ya afya ili kuboresha huduma za afya nchini," amesema Dkt. Mollel.


Aidha, gloves zaidi ya milioni 4 zimetengenezwa tangu kiwanda hicho kifunguliwe Februari mwaka huu. Kiwanda hiki kinatarajiwa kuongeza uzalishaji na kutosheleza mahitaji ya ndani ya gloves, huku kikipunguza gharama za uagizaji wa bidhaa kutoka nje ya nchi.

Kwa upande wake, Kaimu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Afya na Masuala ya UKIMWI, Mhe. Christine Mnzava, amepongeza juhudi hizo za uzalishaji wa gloves na kutoa rai juu ya utunzaji wa rasilimali hizo. 

Pia, amesisitiza umuhimu wa kuweka mazingira rafiki kwa watumishi wa kiwanda hicho ili kuhakikisha wanafanya kazi katika mazingira salama na yasiyoathiri afya zao.


Uwepo wa viwanda kama hivi ni hatua muhimu katika kufanikisha lengo la Tanzania la kujitegemea katika uzalishaji wa vifaa tiba na dawa, na hivyo kuboresha upatikanaji wa huduma bora za afya kwa wananchi kwani, itachangia katika kukuza uchumi wa ndani kupitia ajira na uzalishaji wa ndani, na hivyo kuwa na athari chanya kwa maendeleo ya taifa.