Customer Feedback Centre

Ministry of Health

SERIKALI KUBORESHA UTARATIBU WA LIKIZO YA UZAZI KWA WANAWAKE

Posted on: August 1st, 2024

.


Na. WAF – Dodoma.


Serikali inaendelea na jitihada za kupunguza changamoto za unyonyeshaji kwa wanawake wenye mazingira magumu ya kunyonyesha watoto kutokana na matatizo ya kiafya kwa kufanya marekebisho ya utaratibu wa likizo ya uzazi kwa wanawake wanaojifungua watoto ambao hawajatimiza muda wa kuzaliwa au wenye matatizo makubwa ya kiafya.


Hayo yamesemwa leo Agosti 1, 2024 na Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Tiba kutoka Wizara ya Afya, Dkt. Mwinyi Kondo wakati akimuwakilisha Waziri wa Afya, Mhe. Ummy Mwalimu, kwenye ufunguzi wa maadhimisho ya wiki ya unyonyeshaji duniani, yanayofanyika jijini Dodoma yanayoenda na kauli mbiu isemayo “Tatua Changamoto; Saidia Unyonyeshaji wa Watoto kwa Wote”. 

Dkt. Mwinyi amesema maboresho hayo yatasaidia wanawake kupata muda wa kuwatunza vizuri watoto hao wenye matatizo na kupunguza hatari ya vifo kwa Watoto, pia yatasaidia kulinda ajira za wanawake ambao walikuwa wanapoteza ajira kutokana na kushindwa kurudi kazini baada ya likizo ya uzazi ya kawaida kumalizika.


“Natumia fursa hii kuwahimiza waajiri katika sekta za kiserikali, zisizo za kiserikali na jamii kwa ujumla kusaidia katika kutatua changamoto zinazowakabili wanawake iliwaweze kunyonyesha watoto na waajiri wahakikishe wanatenga sehemu maalum katika eneo la kazi kwaajili ya wafanyakazi wanawake wanaonyonyesha ili Watoto waweze kupata haki zao za kimsingi na kuwa na Afya na lishe bora”. Amesema Dkt. Mwinyi.

Kwa upande wake Kamishna wa Kazi Msaidizi kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi Vijana na Watu wenye Ulemavu Bw. Andrew Ebron amesema Ofisi ya Waziri Mkuu ipo mstari wa mbele kuhakikisha sheria zote zinafuatwa kwa mwanamke na kuhakikisha anapata likizo ya siku 84 kwa mwanamke aliejifungua mtoto mmoja na siku 100 kwa mwanamke aliejifungua mtoto zaidi ya mmoja


Awali akimkaribisha Mgeni Rasmi, Mkurugenzi Msaidizi Huduma za Lishe Bi. Neema Joshua ameeleza kuwa maadhimisho wiki ya unyonyeshaji maziwa ya mama kwa watoto yalianzishwa na kusimamiwa na Shirika la Kuhudumia Watoto (UNICEF) na Shirika la Afya Duniani (WHO) mwaka 1992 duniani kote kwa lengo la kuhakikisha afya za watoto zinakuwa katika hali nzuri na lishe bora


“Tunakutana kila mwaka kwa ajili ya kukumbushana na kusisitizana lakini tunaangalia pia changamoto ambazo zipo na kuzitatua kwasababu changamoto bado zipo na zinahitaji kutatuliwa” Amesema Bi. Neema