Customer Feedback Centre

Ministry of Health

SERIKALI KUANZISHA HOSPITALI MAALUM YA UTENGAMAO

Posted on: September 10th, 2025

NA WAF – DAR ES SALAAM

Serikali imepanga kupanua idadi ya hospitali zinazotoa huduma bobezi za utengamao kwa kuanzisha hospitali maalum ya utengamao mkoani Tabora, ambayo itajumuisha pia huduma za wazee (Geriatric services).

Hayo yamebainishwa leo Septemba 10, 2025 na Mratibu wa Huduma za Tafiti kutoka Ofisi ya Rais TAMISEMI, Dkt. James Kengia, wakati wa ufunguzi wa Kongamano la Utengamao, Jijini Dar es Salaam.

Dkt. Kengia amesema licha ya mpango wa kuanzisha hospitali maalum ya utengamao mkoani Tabora, Serikali inaendelea kuboresha vituo vya afya vilivyopo ili viweze kutoa huduma za utengamao na kuanzisha huduma katika vituo ambavyo kwa sasa havitoi huduma hizo, hususan katika vituo vya huduma za afya ya msingi.

Amesema Serikali imekuwa ikiweka msisitizo mkubwa katika kuhakikisha huduma za afya za utengamao zinakuwa bora na zina uwezo wa kukidhi mahitaji ya Watanzania wote bila kujali hali zao au maeneo wanakoishi, kwani ni sehemu muhimu kwa wagonjwa wanaohitaji huduma za urekebishaji wa viungo, matibabu ya muda mrefu, na msaada wa kisaikolojia ili waweze kurejea katika hali yao ya kawaida.

“Serikali inaendelea kutilia mkazo elimu jumuishi kwa kuandaa mazingira wezeshi ya kufundisha na kujifunza kwa watoto wenye changamoto mbalimbali, kama vile usonji, matatizo ya uoni na usikivu, matamshi (Dyslexia), na hata wale wenye ulemavu wa viungo,” amesema Dkt. Kengia.

Kwa kulitambua hilo amesema, walimu wanawezeshwa ili kutoa elimu inayokidhi mahitaji ya watoto hao, hivyo huduma hizo za utengamao zinatakiwa kuendelea kutolewa si tu kwenye vituo vya huduma za afya pekee, bali pia katika jamii na hata shuleni.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Rihab Health, Dkt. Remla Shirima, amesema huduma hizo ni muhimu kwa matibabu na kusaidia watu wenye maradhi na majeraha ya muda mrefu kurejeshewa hali zao za kawaida na kuboresha maisha yao.

Dkt. Shirima ameziomba sekta binafsi kuunga mkono juhudi za Serikali katika kuhakikisha huduma za utengamao zinapatikana kwa wingi, akiongeza kuwa hamasa kubwa inatokana na kaulimbiu ya Kongamano hilo.