Customer Feedback Centre

Ministry of Health

SERIKALI INATAMBUA MCHANGO WA TIBA ASILI, TIBA MBADALA

Posted on: March 8th, 2025

Na WAF - Dar es Salaam

Serikali imesema inatambua mchango wa watoa huduma za tiba asili na tiba mbadala kwenye utoaji wa huduma za Afya za msingi nchini.

Hayo yamebainishwa na Kaimu Mkurugenzi Msaidizi Sehemu ya Tiba Asili na Tiba Mbadala, kutoka Wizara ya Afya, Dkt. Winifrida Kidima Machi 6, 2025 wakati wa zoezi la Usimamizi Shirikishi uliofanyika Jijini Dar es Salaam.

Kidima amesema mchango huo unaendelea kuonekana na kuwa na tija na ufanisi zaidi iwapo watoa huduma za tiba asili watafuata miongozo na kanuni za Afya katika utoaji wa tiba.

“Dawa za tiba asili zimeendelea kuimarisha afya ya mwili na kutibu magonjwa mbalimbali, hivyo ili tuzidi kufanikiwa ni lazima tufuate miongozo na taratibu zinazotuongoza wakati wa utoaji wa Huduma,” amesema Dkt. Kidima.

Dkt. Kidima ametoa rai kwa watoa huduma kusajili dawa zao kwa zile zinazokidhi viwango vya ubora na usalama.

Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Dkt. Mohamed Mang’una ameomba Wizara kupitia kitengo cha Tiba Asili na Tiba Mbadala kufanya usimamizi shirikishi mara kwa mara hususan kwa mkoa wa Dar es Salaam ili kugundua changamoto za watoa huduma za tiba asili kwa kushirikiana na waratibu wa Mkoa na Wilaya.

“Kwa Wataalam wa tiba asili na tiba mbadala boresheni zaidi maeneo yenu ya ya kutolea huduma kwa kuweka miundombinu sahihi ili kuongeza tija kwa wanufaika wa huduma,” amesema Dkt. Mang’una.

Wizara ya Afya imeendesha zoezi la usimamizi kwa kushirikiana na waratibu wa huduma za afya za tiba asili na tiba mbadala za wilaya tatu za mkoa wa Dar es Salaam katika vituo vilivyopo Wilaya ya Ubungo, Kigamboni na Ilala kabla ya kumalizika Alhamisi ya Machi 06, 2025.