Customer Feedback Centre

Ministry of Health

RAIS SAMIA ATIMIZA AHADI YA KUPELEKA MADAKTARI BINGWA ANJOUAN, COMORO

Posted on: October 2nd, 2025

Na WAF - Comoro

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan ametimiza ahadi ya kuwapeleka madaktari bigwa kutoka nchini Tanzania kwenda katika kisiwa cha Anjouan kilichopo nchini Comoro kwa lengo la kutoa huduma za afya za kibingwa nchini humo.

Balozi wa Tanzania nchini Comoro Mhe. Saidi Yakub amesema hayo leo Oktoba 01, 2025 na kuushukuru uongozi wa kisiwa hicho chini ya Gavana na Wizara za Afya na Mambo ya Nje Comoro kwa kufanikisha mapokezi makubwa ya madaktari hao.

Wakati akiwakaribisha madaktari hao, Gavana wa Kisiwa hicho cha Anjouan, Mheshimiwa Dkt. Youssef Zaidou amesema wataalam hao kutoka Tanzania ni msafara wa kwanza kufika kisiwani humo kwa ajili ya kuweka kambi tiba.

“Tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutimiza ahadi yake kwa wakazi wa kisiwa hicho aliyoitoa kwa Rais wa nchi hiyo Mhe. Azali Assoumani na wananchi wa Comoro alipohudhuria sherehe za Uhuru mwezi Jula 2025,” amesema Gavana Zaidou.

Madaktari hao wametoka katika Taasisi ya Jakaya Kikwete na Hospitali ya Taifa Muhimbili ambao wamewasili tayari na baadaye (wiki hii madaktari) madaktari hao watatoka katika Hospitali ya Benjamin Mkapa, Taasisi za Mifupa na Mishipa ya Muhimbili (MOI) na Taasisi ya Saratani ya Ocean Road wakiambatana na wataalam kutoka Bohari Kuu ya Dawa (MSD).

Huduma zitakazotolewa katika kambi hiyo ni pamoja na kutibu magonjwa ya saratani, macho, meno, moyo, ngozi, figo, matatizo ya uzazi kwa wanawake na wanaume na mifumo ya mkojo.