Customer Feedback Centre

Ministry of Health

PROF. MAKUBI ATAKA VIFAA VYA TEHAMA VIKAONGEZE UFANISI WA HUDUMA ZA MAABARA

Posted on: December 19th, 2022

Na WAF – Dar Es Salaam

Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Prof. Abel Makubi amewataka Watendaji katika Hospitali za kanda waliopata vifaa vya tehama kuhakikisha vinaongeza ufanisi wa huduma za maabara na udhibiti wa ubora wa vipimo.

Prof. Makubi amesema hayo leo jijini Dar Es Salaam wakati akikabidhi vifaa hivyo vya tehama zikiwemo kompyuta na vitunza kumbukumbu (Servers) vilivyotolewa na CDC kupitia Shirika la PATH vyenye thamani ya Shilingi Bilioni moja ambavyo vimetolewa kwa awamu ya kwanza katika Hospitali za kanda za KCMC, Bugando na Hospitali ya Rufaa ya kanda ya Mbeya.

“Tunategemea hivi vifaa vitaongeza ufanisi kwa matumizi ya mifumo ya kielektroniki maabara zetu, lakini pia vitaongeza udhibiti wa ubora wa vipimo kwani hili ni suala la msingi sana ikiwa ni kipaumbele chetu ni ubora wa huduma ikiwemo huduma za uchunguzi,” amesema Prof. Makubi.

Prof. Makubi ameongeza kuwa vifaa hivyo vitasaidia kuchakata mfumo ili majibu yaweze kupatikana katika ubora wake na haraka ili kuepusha usumbufu kwa wananchi kusubiri majibu kwa muda mrefu.

Aidha, amezitaka Hospitali zilizopata vifaa kuhakikisha zinavitunza ili visiweze kuharibika haraka na kuwataka viongozi wa Hospitali hizo kumpelekea taarifa ya utendaji wa vifaa vinavyotolewa kila baada ya miezi sita.

Naye, Mkurugenzi wa shirika la PATH Bw. Amos Mugisha amesema vifaa hivyo vya tehama vitaongeza huduma thabiti za maabara katika kufanya uchunguzi, ufuatiliaji, tiba na kinga dhidi ya magonjwa na uboreshaji kulingana na miongozo ya afya ya kimataifa.