Customer Feedback Centre

Ministry of Health

NPHL YAKABIDHIWA MASHINE MPYA ZA KUBAINI VINASABA VYA VIMELEA

Posted on: September 11th, 2024

Serikali kupitia Wizara ya Afya imeikabidhi Maabara ya Taifa ya Afya ya Jamii mashine mpya tatu za kisasa za kubaini anuwai za vinasaba vya vimelea (Next Generation Sequencers)


Hafla ya makabidhiano hayo imeongozwa na Katibu Mkuu Wizara ya Afya Dkt. John Jingu Septemba 9, 2024 katika Maabara hiiyo iliyopo Mabibo, jijini Dar es salaam. 


Akikabidhi mashine hizo Dkt. Jingu amesema Serikali inatambua na kuthamini kazi kubwa inayofanywa na Maabara hiyo hivyo Vifaa hivyo ni muhimu kuwepo katika maabara hiyo ili kuleta tija kwenye afua mbalimbali zinazofanywa katika maabara hiyo.


Mashine zilizokabidhiwa ni pamoja na mashine moja kubwa ya Illumina NextSeq 1000 kwa ajili ya kuchakata sampuli nyingi na kwa kiwango cha juu, na mashine mbili za iSeq 100 kwa ajili ya Maabara Jongezi (BSL-3 Mobile Laboratories). 


Dkt. Jingu amepongeza juhudi kubwa za Maabara ya Taifa ya Afya ya Jamii kufuatilia na kuthibitisha kwa haraka magonjwa ya mlipuko, hatua inayosaidia kudhibiti kuenea kwa magonjwa na kupunguza madhara kwa jamii.


Kwa upande wake Meneja wa Maabara hiyo Dkt. Nyambura Moremi ameshukuru juhudi zinazofanywa na Serikali pamoja na Wadau wa Sekta ya Afya katika kuboresha huduma katika Maabara hiyo.


Amesema kuwa mbali na kufuatilia magonjwa ya milipuko mashine hizo zinauwezo wa kufuatilia usugu wa vimelea dhidi ya dawa pamoja na kutumika katika tafiti mbalimbali za kiafya kwa lengo la kuboresha afya ya Jamii.