Customer Feedback Centre

Ministry of Health

MTWARA NA MIKOA JIRANI WATAKIWA KUJITOKEZA KWENYE TAMASHA KUBWA LA MZIKI MNENE.

Posted on: July 21st, 2022

Na. WAF - Mtwara

Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Brig. Gen. Marco Gaguti ametoa rai kwa wakazi wa Mkoa huo kujitokeza kwa wingi katika tamasha la mziki mnene litakalofanyika katika viwanja vya Nangwanda Sijaona siku ya Jumamosi Julai, 23, 2022.

Katika Tamasha hilo mgeni rasmi atakuwa Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu na litahusisha wasanii mbalimbali kutoka Tanzania wakiongozwa na msanii wa nyumbani (Mtwara) @harmonize_tz na wananchi hao wataingia kiwanjani hapo bila malipo(Bure).

Tamasha hilo litaongozwa na zoezi la utoaji wa chanjo ya UVIKO-19 kwa wananchi wa Mkoa wa Mtwara katika viwanja vya Nangwanda kwa lengo la kuwakinga wananchi wa Mkoa huo na maambukizi ya virusi vya ugonjwa huo.

Mkoa wa Mtwara ulizindua utoaji wa chanjo ya UVIKO-19 Agosti 03, 2021 kwa lengo la kufikia watu laki nane na themanini (880,000) lakini hadi sasa wamefikia idadi ya watu laki mbili na tisini na tano (295,000) sawa na 33%.

"Tamasha la mziki mnene ni tamasha maalumu lenye lengo madhubuti la kulinda Afya za wananchi wa Mtwara na Afya za watanzania, hivyo niwaalike wana mtwara wote na Mikoa jirani kuja kwenye tamasha hili pamoja na kupata chanjo ya UVIKO-19 ili tuongeze idadi ya waliopata chanjo kwa kujilinda wenyewe na kuwalinda tuwapendao." Amesema Brig. Gen. Gaguti

Aidha, Brig. Gen. Gaguti amewataka wajasiliamali wadogo kutumia fursa hiyo kufanya biashara zenye tija ili kukuza kipato kwa kuwa uchumi unaanza na mtu mmoja mmoja kisha Mkoa na Taifa kwa ujumla.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya Mtwara Mhe. Dunstan Kyobya amewahakikishia wana Mtwara kuwa na ulinzi wa kutosha na usalama katika tamasha hilo.

"Tamasha letu litakwenda vizuri kama tulivyo panga, na taratibu zote zitatolewa wapi tunaanzia mbio zetu na tunamalizia wapi hivyo tumejipanga vizuri kupitia kamati yangu ya usalama kuhakikisha usalama wa wananchi katika wilaya hii unakua vizuri."Amesema Bw. Kyobya