Customer Feedback Centre

Ministry of Health

MSAJILI BARAZA LA OPTOMETRIA AISHAURI HOSPITALI YA KOLANDOTO KUREJESHA HUDUMA ZA MKOBA ZA MACHO

Posted on: February 25th, 2025

Na WAF - SHINYANGA

Msajili wa Baraza la Optometria nchini, Bw. Sebastiano Millanzi kwa kushirikiana na Ofisi ya Mganga Mkuu wa Mkoa Shinyanga ameendesha usimamizi shirikishi katika mkoa huo na kuwataka wamiliki wa vituo vinavyotoa huduma za optometria vinafuata miongozo chini ya sheria zilizopo.

Bw. Millanzi ametoa kauli hiyo Februari 24, 2025 mkoani Shinyanga wakati wa zoezi la ufuatiliaji shirikishi wa vituo unaolenga kuboresha huduma za optometria kwa wananchi na kuhakikisha kila kituo kinazingatia taratibu za kitaalamu na usalama wa wagonjwa.

"Hospitali ya Kolandoto inajulikana kwa historia yake katika utoaji wa huduma za afya ya macho, ikiwa ni miongoni mwa vituo vilivyokuwa vinatoa huduma za mkoba kwa jamii za vijijini kwa miaka mingi hivyo rudisheni huduma hizi hili muweze kuwafikia wananchi walipo" amesema Bw. Millanzi.

Bw. Millanzi amefafanua kuwa uongozi wa Hospitali ya Kolandoto ni vema ikaliona hilo la kurejesha huduma za mkoba, akisisitiza kuwa ni muhimu kuwafikia wananchi wa maeneo ya pembezoni ambako huduma za macho bado ni changamoto.

"Mkirejesha huduma hizi za mkoba za macho itaimarisha Hospitali yenu kama kituo cha rufaa cha huduma za macho na kusaidia kupunguza mzigo kwa hospitali kubwa za mkoa na taifa kama mnavyofahamu Serikali imeweka mazingira wezeshi kwa sekta binafsi kuboresha huduma za afya katika nchini" amesisitiza Bw. Millanzi.

Aidha, Bw. Millanzi akiwa katika ziara hiyo shirikishi ametembelea Kitengo cha macho kilichopo katika Hospitali ya Mkoa wa Shinyanga, kituo cha Charity Optometrist Eye Care, Mtoke Investiment and Ophthalmological Service vyote vya mjini Shinyanga na kuwapa elimu na ushauri wa optometria.

Usimamizi huu umebaini changamoto mbalimbali za upatikanaji wa miwani bora na uhaba wa vifaa vya uchunguzi vya optometria, hali inayosababisha wagonjwa wengi kushindwa kupata huduma wanazohitaji kwa haraka hata kuhatarisha usalama wa macho yao.