Customer Feedback Centre

Ministry of Health

MIREMBE YAZINDUA KAMPENI KITAIFA“ AFYA YA AKILI NI AFYA”

Posted on: May 8th, 2025

Na WAF, Dodoma

Kaimu Mganga Mkuu wa Serikali Bi. Ziada Sellah amezindua rasmi Kampeni ya kitaifa ya Afya ya Akili ni Afya, yenye lengo la kuongeza uelewa juu ya afya ya akili nchini ili kuhakikisha kila mwananchi ana ustawi wa akili.

Uzinduzi huo umefanyika leo Mei 7, 2025 jijini Dodoma Katika Hospitali ya Taifa ya Afya ya Akili Mirembe ambapo kampeni ya kitaifa ya "AFYA YA AKILI NI AFYA", ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Mwezi wa Uhamasishaji jamii juu ya uelewa wa Afya ya Akili (Mental Health Awareness Month) unaoadhimishwa mwezi Mei kila mwaka.

Bi. Ziada amesema Kampeni hii inalenga kuhamasisha jamii nzima kuhusu umuhimu wa afya ya akili kama sehemu muhimu ya afya ya binadamu kwa ujumla.

“Kauli mbiu hii ina ujumbe mzito: “Afya ya akili ni afya”, hivyo hatuwezi kuwa na jamii yenye nguvu bila kuhakikisha kila mmoja ana ustawi wa akili, ”ameaema Bi. Ziada.

Amesema kuwa Afya ya akili ni kichocheo muhimu cha maendeleo ya jamii na uchumi ambapo amesema bila afya ya akili iliyo imara, hakuna ufanisi kazini, hakuna furaha katika familia na hakuna mshikamano katika jamii.

Ameeleza kupitia kampeni hiyo, wanataka kuondoa unyanyapaa, kuhamasisha mazungumzo ya wazi kuhusu changamoto za afya ya akili na kuhakikisha kila mwananchi anapata huduma bora bila hofu wala unyanyapaa.

Tunaelewa kuwa changamoto za afya ya akili zinatokana na sababu mbalimbali za kibaiolojia, kisaikolojia, kijamii na kiuchumi, kwa mfano, umasikini, ukosefu wa ajira, magonjwa sugu, na majanga kama COVID-19 yameongeza kwa kiasi kikubwa mzigo wa changamoto za afya ya akili katika jamii yetu.

Ameongeza kuwa takwimu zinaonesha kuwa magonjwa kama sonona (depression), wasiwasi (anxiety) na utegemezi wa dawa za kulevya yanazidi kuongezeka, huku Shirika la Afya Duniani likikadiria kuwa mtu mmoja (1) kati ya wanne (4) duniani anakumbwa na tatizo la afya ya akili katika maisha yake.