Customer Feedback Centre

Ministry of Health

MICHEZO YA KUBAHATISHA, BIDHAA ZA UREMBO, VINYWAJI LAINI NA VILEO KUCHANGIA MFUKO WA BIMA YA AFYA KWA WOTE.

Posted on: June 13th, 2024


Serikali imepanga Kutoza Ushuru wa Bidhaa kwa kiwango cha asilimia 10 kwenye thamani ya dau la kamari (value of the stake on betting) kwenye Michezo ya Kubahatisha na Bahati Nasibu ya Taifa ili Mapato yatakayokusanywa kutoka chanzo hiki yatumike kugharamia bima ya afya kwa watu wasio na uwezo na makundi maalum hususan wanawake wajawazito na watoto wa umri chini ya miaka mitano.


Hayo yameelezwa Leo Juni 13, 2024 Bungeni Jijini Dodoma na Waziri wa Fedha Dkt. Mwigulu Nchemba wakati akiwasilisha Bajeti kuu ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2024/25 Sheria ya Ushuru wa Bidhaa, SURA 147

ambapo amesema Hatua hiyo inatarajia kupeleka kiasi cha shilingi milioni 29,522 katika Mfuko wa Bima ya Afya.


Dkt. Mwigulu ameongeza kuwa Serikali imefanya marekebisho kwenye Sheria ya Ushuru wa Bidhaa, Sura 147 ili kuelekeza asilimia 2 ya mapato ya Ushuru wa Bidhaa yanayokusanywa kutoka kwenye bidhaa za urembo, vinywaji laini (carbonated drinks) na vileo (bia na pombe kali) kwenye Bima ya Afya kwa wote.


”Lengo la hatua hii ni kuongeza fedha zitakazotumika kwa ajili ya kugharamia bima ya afya kwa watu wasio na uwezo na makundi maalum hususan wanawake wajawazito na watoto wa umri chini ya miaka mitano. Hatua hii inatarajia kupeleka kiasi cha shilingi milioni 18,800 katika Mfuko huo” amesema Dkt. Mwigulu.


Amesema pia Serikali itatoza mapato ya Serikali kwa kiasi cha shilingi milioni 634, Kutoza Ushuru wa Bidhaa kwa kiwango cha Shilingi 500 kwa kilo moja ya rangi za mafuta (solvent based paints and vanishes) zinazotoka nje ya nchi. Rangi hizo zinatambulika kwa heading 32.08. Lengo la hatua hii ni kuongeza mapato ya Serikali na kupata fedha za fidia ya athari hasi zinazotokana na matumizi ya bidhaa hizo. Hatua hii inatarajia kuongeza mapato ya Serikali kwa kiasi cha shilingi milioni 2,433.