MIAKA MINNE YA RAIS SAMIA SERIKALI YALIPA SHILINGI TRILIONI 2.3 VITUO VYA AFYA
Posted on: March 11th, 2025
Na WAF - DODOMA
Serikali imelipa Shilingi Trilioni 2.3 kwa vituo vya afya ili kugharamia huduma za bima ya afya, hatua inayoonesha jitihada za kuimarisha upatikanaji wa matibabu kwa wananchi.
Hayo yameelezwa leo, Machi 10, 2025, na Mkurugenzi wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), Dkt. Irene Isaka, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma, kuhusu mafanikio na mwelekeo wa Mfuko huo kwa kipindi cha miaka minne (4) ya Serikali ya Awamu ya Sita.
“Lengo la Serikali ni kuhakikisha kila Mtanzania anakuwa na bima ya afya ili kupata huduma za matibabu kwa uhakika hivyo ili kufanikisha hilo, mwaka 2023, Rais, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan alisaini Sheria ya Bima ya Afya kwa Wote itakayowezesha kila Mtanzania kupata huduma ya afya bila kujali hali ya kiuchumi,” amesema Dkt. Isaka
Dkt. Isaka amefafanua kuwa vifurushi vya NHIF vimeboreshwa ili kuendana na upatikanaji wa huduma za kibingwa na Ubingwa bobezi, hatua inayolenga kuboresha huduma kwa wanufaika wa bima ya afya.
“Kwa sasa, asilimia 60 ya fedha zilizotolewa zinatumika kugharamia matibabu ya magonjwa yasiyoambukiza," amesema Dkt. Isaka.
Aidha, Dkt. Isaka amebainisha kuwa NHIF imefanikiwa kuondoa nakisi ya Shilingi Bilioni 120 na kwa sasa ina akiba ya Shilingi Bilioni 95, jambo linaloashiria uimarikaji wa Mfuko huo kifedha.
“Ili kuboresha huduma kwa wanachama, NHIF inashirikiana na sekta binafsi kwa pamoja ili kuongeza idadi ya wanachama wapya,” amesema Dkt. Isaka
Pia, Mfuko huu unashirikiana na Ofisi ya Rais TAMISEMI kutambua kaya zenye uhitaji wa bima ili kuhakikisha kila mwananchi mwenye uhitaji anapata huduma za afya kwa urahisi.
Dkt. Kisaka ametoa wito kwa waandishi wa habari kushirikiana na NHIF ili kuwaelimisha na kuwahamasisha wananchi kuhusu faida za kuwa na bima ya afya.