Customer Feedback Centre

Ministry of Health

MBINU ZAIDI ZAHITAJIKA KUFIKISHA ELIMU YA AFYA NGAZI YA JAMII

Posted on: October 22nd, 2023

Na WAF - DODOMA 


Serikali imewaasa wadau wa Afya Nchini kubuni mbinu zitakazowezesha elimu ya Afya kufikia makundi mbalimbali katika jamii hususani wasichana na wavulana walio katika umri balehe ili kufikia malengo ya Kidunia ya TISINI TANO TATU yenye lengo la kupunguza kasi ya maambukizi mapya ya VVU ifikapo 2030.


Hayo yamebainishwa na Katibu Tawala Msaidizi wa Mkoa wa Dodoma Dkt. Best Magoma Wakati akimuawakilisha Mkuu wa Mkoa huo Mhe. Rosemary Senyamule katika Uzinduzi wa jukwaa la Jikubali linaloratibiwa na Wizara ya Afya kupitia Mpango wa Taifa wa Kudhibiti UKIMWI kwa ufadhili wa The Global Fund, NACP na EFM, Oktoba 22 katika Viwanja vya Chinangali, Jijini Dodoma.


Dkt. Magoma amewasihi Walimu kuja na njia zitakazo weka msisitizo wa ziada katika kutoa elimu ya afya shuleni na kuwasaidia watoto wanaoishi na maambukizi ya VVU bila ya kuwanyanyapaa. 


"Kampeni hii inaenda sambamba na jitihada za nchi yetu katika kufikia malengo ya Kidunia ya TISINI TANO TATU (95 95 95) ambayo tuliyaridhia mwaka 2015. Malengo ya TISINI TANO TATU yana matarajio ya kuhakikisha kuwa ifikapo mwaka 2030, asilimia 95 ya watu wanaoishi na VVU wawe wamepimwa na kujua hali zao za maambukizi ya VVU". Amesema Dkt. Magoma.


Dkt. Magoma ameongeza kuwa Jukwaa la Jikubali ni moja ya bunifu zitakazojenga uelewa sahihi kuhusu masuala ya Afya ya uzazi na VVU, jambo ambalo litawawezesha vijana kujiepusha na vishawishi. 


"Kampeni hii pia imelenga kuwafanya Vijana wasiyape kipaumbele masuala ya ngono mapema hivyo kujiepusha na mimba za utotoni pamoja na magonjwa ya ngono ikiwemo maambukizi ya VVU". Aliongeza Dkt. Magoma.


Kwa upande wake Meneja wa Mpango wa Kudhibiti UKIMWI kutoka wizara ya Afya Dkt. Anath Rwebemberwa amesema takwimu zinaonesha mpaka sasa nchini juna maambukizi Milioni 1.7, jambo linalochochea jukumu la kuhakikisha maambukizi hayaongezeki na wanafubaza makali ya ugonjwa huo kwa maambukizi ya awali.


Nuraty Aboubakari kutoka Iyumbu Sekondari Ni miongoni mwa Wanafunzi walioshiriki uzinduzi wa kampeni ya Jikubali, akizungumza kwa niaba ya wanafunzi wengine amesema Moja ya makundi yaliyo nyuma katika kufikia malengo ya TISINI TANO TATU ni kundi la VIJANA. Kwani vijana wengi wenye umri wa miaka 15 -24 hawajui hali zao za maambukizi ukilinganisha na watu wenye umri mkubwa.