Customer Feedback Centre

Ministry of Health

MAZIWA YA MAMA NI KINGA DHIDI YA MAGONJWA KWA MTOTO

Posted on: July 30th, 2025

Na WAF – Dar es Salaam


Jamii imeaswa kuzingatia afya za watoto wachanga kwa kutoa nafasi ya mapumziko kwa wanawake waliopo katika sekta rasmi na isiyo rasmi ili waweze kuwanyonyesha kikamilifu watoto wao kwa kutumia maziwa ya mama kama inavyopendekezwa na wataalamu wa afya.


Hayo yamebainishwa leo, Julai 30, 2025, jijini Dar es Salaam na Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais – TAMISEMI (Afya), Prof. Tumaini Nagu, wakati wa akifungua maadhimisho ya Wiki ya Unyonyeshaji wa Maziwa ya Mama Duniani pamoja na uzinduzi wa Mwongozo wa Kitaifa wa Kuzuia na Kutibu Ukondefu (Wasting) na Uvimbe unaotokana na Ukondefu (Nutritional Oedema) kwa watoto walio chini ya umri wa miaka mitano jijini Dar es Salaam. 


Prof. Nagu amesema kuwa, kwa kuzingatia taratibu zilizotolewa na Shirika la Afya Duniani (WHO), watoto wanapaswa kupewa uangalizi wa karibu na kunyonya maziwa ya mama ipasavyo ili kuboresha afya na kuwakinga dhidi ya magonjwa yatokanayo na ukosefu wa virutubisho muhimu vilivyomo kwenye maziwa ya mama.


“Miongozo inatuelekeza kwamba mtoto anatakiwa aanze kunyonya maziwa ya mama ndani ya saa moja baada ya kuzaliwa, aanze kula vyakula vingine akifikishapo miezi sita, lakini bado aendelee kunyonya hadi atakapofikisha miaka miwili, kwa sababu maziwa ya mama yana virutubisho vyote muhimu na hutoa kinga dhidi ya magonjwa,” amesema Prof. Nagu.


Naye Mkurugenzi wa Shirika la Action Against Hunger Tanzania, Bw. Zacharia Imeje, amesema uzinduzi wa mwongozo huo utawasaidia wahudumu wa afya, ambao ndio watu wa karibu na watoto, kushughulikia changamoto za lishe duni na ukondefu kwa ufanisi zaidi.


“Sisi kama taifa tunaweza kushughulikia mahitaji ya lishe kwa watoto wetu kwa njia bora. licha ya muda uliotumika kuukamilisha mwongozo huu, tuna furaha kwamba sasa umeidhinishwa na Wizara ya Afya. Tunatarajia wadau wote wanaoshughulika na utapiamlo watautumia kwa manufaa mapana ya afya za watoto wa Kitanzania,” alisema Bw. Imeje.


Takwimu zinaonesha kuwa viwango vya unyonyeshaji wa watoto nchini Tanzania vinaendelea kuimarika kwani Idadi ya watoto wanaonyonyeshwa maziwa ya mama pekee imeongezeka kutoka asilimia 58 mwaka 2018 hadi asilimia 64 mwaka 2022. 


Aidha watoto wanaonyonyeshwa ndani ya saa moja baada ya kuzaliwa wameongezeka kutoka asilimia 53.5 mwaka 2018 hadi asilimia 70 mwaka 2022, huku watoto wanaoendelea kunyonya hadi umri wa miaka miwili au zaidi wakiwa ni asilimia 62.