MATUMIZI YA TAKWIMU YACHANGIA KUIMARISHA HUDUMA ZA AFYA NCHINI
Posted on: October 4th, 2025
Na WAF, Dar es Salaam
Serikali imejidhatiti kuendelea kushirikiana na Wadau wa Sekta ya Afya katika matumizi ya takwimu na teknolojia ili yaweze kuleta tija katika kuimarisha mifumo ya sekta ya afya nchini hivyo kuchangia katika uboreshaji wa huduma za afya kwa wote.
Hayo yamesemwa na Mganga Mkuu wa Serikali Dkt. Grace Magembe leo Oktoba 03, 2025 wakati akihitimisha Mkutano wa 12 wa Afya Tanzania (THS) uliofanyika kwa siku tatu katika Ukumbi wa mikutano wa Mwalimu Julius Nyerere jijini Dar es Salaam, na kuhudhuriwa na wajumbe zaidi ya 1,700 kutoka ndani na nje ya nchi.
“‘Data’ siyo tena anasa, bali ni hitaji la msingi na ndio inayotuongoza kuamua wapi pa kuelekeza rasilimali tulizo nazo kwa kiasi gani na kwa wakati upi kwani bila data, huna haki ya kuzungumza,” amesema Dkt. Magembe.
Dkt. Magembe amebainisha kuwa jamii ndio msingi wa mfumo wa afya na kwamba kila ubunifu unaojadiliwa katika vikao hivyo lazima ubadilishwe kuwa maboresho ya moja kwa moja katika huduma za afya ngazi ya msingi.
“Huduma za afya ngazi ya msingi ndizo uti wa mgongo wa mfumo wowote wa afya, hatuwezi kuwa na mfumo imara wa afya kama huduma za afya ngazi ya msingi ni dhaifu,” amesema Dkt. Magembe.
Aidha Dkt. Magembe amesema Serikali itaendelea kuweka mazingira wezeshi ya kisera yatakayohamasisha uwekezaji katika sekta ya afya, haswa katika mifumo ya kidijitali na uboreshaji wa huduma endelevu.
"Niwahakikishie kwamba tutaendelea kuunga mkono kazi zinazofanywa na Tanzania Health Summit (THS) pamoja na wadau wote waliopo hapa na naamini tuna mengi ya kujifunza kutoka kwa kila mmoja," amesema Dkt. Magembe.
Pia amewapongeza wajumbe wote kwa mijadala yenye tija na kuwataka kila mmoja anaporudi katika maeneo yake ya kazi awe chachu ya mabadiliko ya kiutendaji kwa wengine.