Customer Feedback Centre

Ministry of Health

MATUMIZI YA TAKWIMU, MUHTASARI WA SERA KIUNGO MUHIMU UBORESHAJI HUDUMA ZA AFYA NCHINI

Posted on: December 20th, 2024


Na WAF - Dar es Salaam.

Serikali kupitia Wizara ya Afya na Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), imeendelea kufanya jitihada Mahsusi za kutekeleza afua mbalimbali za kuwajengea uwezo watoa huduma zinazolenga kuboresha hali ya utoaji wa huduma za afya nchini na ili kufikia hilo matumizi ya takwimu na muhtasari wa sera yametakiwa kuwa kiungo muhimu kusaidia Serikali katika kufanya maamuzi ya sekta ya afya.

Hayo yamebainika Disemba 19, 2024 Jijini Dar es Salaam wakati wa mafunzo ya namna ya kuchakata takwimu za afya na kutengeneza muhtasari wa sera, yaliyowakutanisha wataalam wa Wizara ya afya na Ofisi ya Rais-TAMISEMI kutoka maeneo mbalimbali nchini.
 
Mwakilishi kutoka Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Bw. Ally Kananika amesema Serikali inawekeza katika kuwajengea uwezo watoa huduma na wataalam wa sekta ya afya ili kuboresha matumizi ya takwimu.

“Wizara ya Afya kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais-TAMISEMI imeandaa mafunzo haya ili kuwawezesha wataalam kuandaa muhtasari wa Sera utakaowawezesha watumishi na wataalam wa afya kuwa na uwezo wa kuchakata takwimu katika vituo vya afya, ambazo zitasaidia kuonesha mwelekeo wa sekta ya afya,” amesema Bw. Kananika.

Kwa upande wake Mratibu wa mafunzo hayo yaliyofadhiliwa na shirika la CDC Foundation, Dkt. Julius Masaka amesema lengo ni kutengeneza wataalam ambao watakuwa na ujuzi wa kuchakata takwimu na kutengeneza muhtasari wa Sera ambayo itasaidia kukabiliana na changamoto katika sekta ya afya nchini.

“Katika kipindi hiki ambacho tumefanya mafunzo mara tatu na kuwashirikisha zaidi ya watumishi 30 kutoka mikoa mbalimbali nchini, tunawaandaa wao kuwa wakufunzi katika maeneo yao ya kazi,” amesema Dkt. Masaka.

Akizungumza kwa niaba ya wanufaika wa mafunzo hayo Dkt. Calvis Ndato amesema mafunzo hayo yamekuwa dira itakayowawezesha kuja na sera mbalimbali za afya za kukabiliana na changamoto za afya za kijamii.