MATUMIZI YA DATA NA TEKNOLOJIA YAIMARISHA HUDUMA ZA AFYA NCHINI
Posted on: October 2nd, 2025
Na. WAF, Dar es Salaam
Serikali ya Awamu ya sita chini ya Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan imepiga hatua kubwa katika matumizi ya data na ubunifu ili kurahisisha utoaji wa huduma za afya nchini.
Hayo yamesemwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Dkt. Seif Shekalaghe leo Oktoba 01, 2025 wakati akifungua Mkutano wa 12 wa Afya Tanzania (THS) unaofanyika kwa siku tatu katika Ukumbi wa Mikutano wa Mwalimu Julius Nyerere, jijini Dar es Salaam.
Dkt. Shekalaghe amesema Serikali imekumbatia kikamilifu kaulimbiu ya matumizi ya Data na Teknolojia katika kuongeza kasi ya upatikanaji wa huduma za afya kwa wote kwa kuwekeza katika mifumo ya data na teknolojia mpya ili kubadilisha utoaji wa huduma za afya na kusogeza karibu upatikanaji wa huduma za afya kwa wananchi wote.
"Kwa mara ya kwanza katika historia ya nchi yetu, sasa tuna mfumo jumuishi wa rekodi za matibabu za kielektroniki unaounganisha taarifa za mgonjwa kuanzia ngazi ya jamii, vituo vya afya, hospitali za wilaya mpaka taifa," amesema Dkt. Shekalaghe.
Pia. Dkt.Shekalaghe amesema Serikali inajivunia mfumo wa kidigitali wa M-Mama ambao unaratibu usafiri wa dharura kwa mama wajawazito na watoto wachanga walioko kwenye hatari, kupitia namba 155 bila malipo.
"Kama mfumo rasmi wa kitaifa wa usafiri wa dharura wa kina mama, M-mama sasa unahudumia mikoa yote ya Tanzania na unatarajiwa kusafirisha wanawake na watoto wachanga 50,000 kila mwaka kupata huduma wanazohitaji.
Aidha Dkt. Shekalaghe amewahimiza washirika na wadau wote waliohudhuria katika mkutano huo kuendelea kuunga mkono kwani mkutano huo si mkutano wa kila mwaka tu bali umekuwa jukwaa kuu la afya nchini Tanzania mahali pa mawazo, ushirikiano, na uwajibikaji.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Kinga na Elimu ya Afya Zanzibar akimuwakilisha Katibu Mkuu wa wizara hiyo, amesema Serikali ya Mapinduzi Zanzibar inajivunia mafanikio ya
kisekta kupitia mchango mkubwa wa wadau wa afya katika matumizi sahihi ya data na teknolojia kuboresha huduma za afya.