Customer Feedback Centre

Ministry of Health

MASHINE YA UCHUNGUZI, TIBA YA MASIKIO, PUA NA KOO KUTUMIKA SINGIDA

Posted on: February 10th, 2025

Na WAF - SINGIDA

Hospitali Rufaa ya Mkoa wa Singida iko mbioni kuanza kutumia mtambo wa kisasa wa uchunguzi na tiba kwa ajili ya masikio, pua na koo kwa njia ya kamera ujulikanayo kama ENT - TREATMEMT UNIT.

Hayo yamebainishwa na Daktari Bingwa wa Masikio, Pua na Koo wa hospitali hiyo Dkt. Deus Nzela Februari 7, 2025, mbele ya timu ya wataalam toka Wizara ya Afya ambao wameendesha zoezi la usimamizi shirikishi katika hospitali hiyo na kwamba mashine hiyo itafanya uchunguzi na tiba za hali ya juu ambazo awali walikuwa hawafanyi.

Dkt. Nzela amebainisha kuanza kazi kwa mashine hiyo kutaisadia jamii ya Singida na maeneo ya jirani kupata huduma bora na za kibingwa za masikio, pua na koo ambazo awali ziliwalazimu kuzifuata Hospitali ya Kanda ya Benjamin Mkapa iliyopo Dodoma au kwenda Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.

Ameongeza kuwa hospitali hiyo bado inaendelea na jitihada za kuhakikisha mashine hiyo inaanza kufanya kazi Februari hii kwani zoezi lililobakia ni kuunganishwa tu baadhi sehemu ambazo zipo tayari.

Kwa upande wake Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Tiba kutoka Wizara ya Afya, Dkt. Mwinyi Kondo, amesema hatua hiyo ni muendelezo wa azma ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kuhakikisha kila Mtanzania anakuwa na uhakika wa huduma bora na za kibobezi na kutatua changamoto ya kiafya itakayojitokeza.

Dkt. Mwinyi ameongeza kuwa uwekezaji katika mashine hizo unaendelea na kwa sasa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Singida inakuwa na mashine hiyo baada ya Hospitali ya Kanda ya Benjamini Mkapa na Hospitali ya Rufaa ya Maweni, Kigoma.