Customer Feedback Centre

Ministry of Health

MARUFUKU KUDANGANYA UPANGAJI WATUMISHI NGAZI YA JAMII

Posted on: June 12th, 2024



Na WAF, MBEYA


Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Mhe. Benno Malissa amewataka Viongozi katika mkoa huo kuepuka vitendo vya dhuluma, rushwa na udanganyifu wakati wa mchakato wa kuwapata Wahudumu wa Afya Ngazi ya Jamii.


Mhe. Malissa ametoa wito huo wakati akizungumza kwenye semina elekezi kwa Viongozi na Wataalamu wa Mkoa na Wilaya ya Mbeya, Kyela na Chunya juu ya utekelezaji wa Mpango Jumuishi wa Wahudumu wa Afya Ngazi ya Jamii.


“Jambo hili la Mpango jumuishi wa Wahudumu wa Afya Ngazi ya Jamii ni muhimu kwani ndio wasaidizi wakubwa kwenye masuala ya afya, hivyo katika mchakato wa kuwapata pasitokee vitendo vya dhuluma na udanganyifu wapatikane kwa haki”amesema Malissa.


Kwa upande wake Mwakilishi kutoka Wizara ya Afya Bi. Magdalena Dinawi amesema Wizara ya Afya inatambua mchango mkubwa unaofanywa na Wahudumu wa Afya Ngazi ya Jamii ikiwemo utoaji wa Elimu ya Afya hivyo moja ya sifa muhimu ya Mhudumu wa Afya ngazi ya Jamii ni kutoka katika mtaa, kitongoji na Kijiji husika.


Mhe. Malissa ametumia fursa hiyo kuipongeza Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayoongozwa na Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutambua mchango mkubwa wa Wahudumu wa Afya ngazi ya Jamii na kuzindua Mpango Jumuishi wa Wahudumu wa Afya Ngazi ya Jamii kwani wana mchango mkubwa.


MWISHO