Customer Feedback Centre

Ministry of Health

MARUFUKU HOSPITALI KUZUIA MAITI KWA NDUGU WA MAREHEMU

Posted on: January 20th, 2024

Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu amezitaka Hoslitali zote za Umma kutekeleza kwa ukamilifu maelekezo yaliyokwisha tolewa na Serikali ya Marufuku Hospitali kuzuia miili ya marehemu kwa kigezo cha kushindwa kulipa deni la gharama za Matibabu.

Waziri Ummy ametoa agizo hilo wakati akijibu swali la katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama Cha Mapinduzi Paul Makonda katika mkutano wa hadhara uliofanyika jijini Tanga Januari 20, 2024. lililouliza ni upi mkakati wa Serikali wa kuwasaidia wananchi maskini wanaoshindwa kulipia gharama za matibabu kwa kudaiwa kulipia maiti ili hali hawana Uwezo wa kilipa deni na kukomboa mwili.

"Naomba nitumie mkutano huu kuzitaka hospitali zote za serikali, marufuku kuzuia maiti ya mtanzania wowote, haya ndio maelekezo ya Serikali, nawataka Waganga Wafawidhi wa Hospitali zote za Serikali nchini kuzingatia muongozo wa Serikali wa kutozuia maiti, tafuteni njia nyingine, toeni maiti wakizika mtakuja kudaiana mambo mengine" amesema Waziri Ummy.

Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu ametoa rai kwa viongozi wa Mikoa na Wilaya nchini kote kutosita kuwachukulia hatua kwa baadhi ya watendaji na watoa huduma za afya ambao watakiuka maadili, miiko, Miongozo na melekezo ya serikali katika kutoa huduma za Afya.

"Tunataka kuhakikisha watendaji wa wilaya na mikoa wanawajibika kwa utoaji wa huduma za afya katika maeneo yao, kauli yangu ni kwa watumishi wa afya ambao wanakwenda kinyume na miongozo na maelekezo ya serikali wachukuliwe hatua mara moja na viongozi wa Wilaya na Mikoa pale ambapo watabainika kufanya uzembe" amesema Waziri Ummy.