MADAKTARI BINGWA WATOA MAFUNZO YA HUDUMA KWA MAMA NA MTOTO, ITIGI
Posted on: May 1st, 2025
NA WAF - SINGIDA
Timu ya Madaktari Bingwa na Bobezi wa Rais Samia kutoka mikoa mbalimbali wametoa mafunzo ya kuboresha utoaji huduma kwa mama na watoto wachanga kwa watumishi wa afya wa Hospitali ya Wilaya ya Itigi, kwa shabaha yakuwaajengea uwezo watoa huduma wa Halmashauri hiyo.
Mafunzo haya yamefanyika Aprili 30, 2025, na kuongozwa na Dkt. Emmanuel Chogo, Daktari Bingwa wa Watoto, mafunzo yaliyolenga kuongeza ufanisi wa huduma hizo.
“Mafunzo haya ni sehemu ya mikakati ya Serikali ya kuboresha huduma za afya kwa wananchi na kuhakikisha kila kituo cha afya kina wataalam waliobobea na kuwa na weledi stahili kwenye utoaji huduma,” amesema Dkt. Chogo.
Dkt. Chongo amesisitiza kuwa ni muhimu kila mhudumu wa afya kuwa na ujuzi wa kisasa ili kuboresha huduma za tiba kwa wagonjwa ikiwemo pia watoto ambao wanahitaji uangalizi wa kipekee.
Serikali chini ya uongozi imara wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imewekeza vya kutosha katika miundombinu na vifaa tiba vya kisasa, nasi tunafanya kazi kwa karibu kuhakikisha kila kituo cha afya kina wataalam waliobobea na wenye mafunzo ya kutosha ili kuboresha afya ya wananchi kwa ujumla,” amesema Dkt. Chogo.
Pia, Dkt. Chogo amebainisha umuhimu wa watoa huduma kujua jinsi ya kutumia vifaa tiba kwa usahihi na kubainisha kuwa vifaa hivyo vina uwezo mkubwa wa kuboresha matibabu endapo vitatumika ipasavyo na kusaidia wananchi wa maeneo hayo.
Mafunzo haya yatawawezesha wataalam katika vituo vya kutolea huduma za afya kujifunza mbinu bora za kutumia teknolojia na vifaa vya kisasa ili kutoa huduma bora zaidi kwa wagonjwa na kupunguza rufaa zisizo za lazima.