Customer Feedback Centre

Ministry of Health

MADAKTARI BINGWA WA RAIS SAMIA KUTOA HUDUMA 16 ZA KIBINGWA SINGIDA RRH

Posted on: May 5th, 2025

Na WAF - Singida

Katibu Tawala Mkoa wa Singida Dkt. Fatuma Mganga amewataka wananchi mkoani humokujitokeza kwa wingi kupata matibabu kutoka kwa Madaktari Bingwa wa Dkt. Samia waliweka kambi katika Hospitali ya Rufaa ya mkoa huo ili kupata huduma bora za kibingwa na ubingwa bobezi kwa unafuu na ukaribu zaidi.

Wakazi Mkoa wa Singida na maeneo ya jirani wanatarajiwa kunufaika na huduma 16 za kibingwa na ubingwa bobezi ambazo zinatarajiwa kutolewa na Madaktari bingwa kutoka Hospitali za Rufaa za Mikoa ya Dodoma, Morogoro, Pwani na Iringa wakishirikiana na mwenyeji Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Singida watatoa huduma za matibabu.

Hayo yamebainishwa leo Mei 5, 2025 na Katibu Tawala Mkoa wa Singida Dkt. Fatuma Mganga wakati wa uzinduzi wa kambi rasmi ya madaktari bingwa wa Dkt. Samia inayoendelea katika hospitali za Mikoa ambayo itafanyika kuanzia tarehe 5 hadi 9 Mei 2025 mkoani humo.

Dkt. Mganga amesema huduma 16 za kibingwa na bingwa bobezi zinatarajiwa kutolewa na Madaktari bingwa kutoka Hospitali za Rufaa za Mikoa ya Dodoma, Morogoro, Pwani na Iringa wakishirikiana na mwenyeji Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Singida.

Ameongeza kuwa huduma zinazotolewa ni kutoka kwa Madaktari bingwa na bingwa bobezi 55 wenye fani 16 za magonjwa ya Ndani, Magonjwa ya Wanawake na Uzazi, Magonjwa ya Watoto, na Magonjwa ya Upasuaji.

Huduma nyingine ni Ubingwa wa Upasuaji Mifupa, Magonjwa ya Njia ya Mkojo, Magonjwa ya Macho, Magonjwa ya Sikio, Pua Na Koo, na Urekebishaji wa Kinywa Na Meno.

"Wito wangu kwa wananchi ni kuendelea kujitokeza kwa wingi katika Kambi ya matibabu ya Madaktari Bingwa wa Dkt. Samia iliyotia kambi katika Hospitali hiyo ili kupata huduma bora za kibingwa na ubingwa bobezi kutoka kwa Madaktari ", amesema Dkt. Fatuma.

Kambi hiyo imeanza kutoa matibabu kwa wananchi na itadumu kwa siku tano huku ikihusisha Madaktari bingwa na ubingwa bobezi zaidi ya 56 kutoka hospitali mbalimbali za Rufaa ikiwemo hospitali ya rufaa ya Dodoma, Morogoro, Tumbi na Iringa ambao watatoa huduma zote za kimatibabu katika kambi.