Customer Feedback Centre

Ministry of Health

MADAKTARI BINGWA 50 WA RAIS SAMIA WAWEKA KAMBI SINGIDA

Posted on: April 28th, 2025

Na WAF-SINGIDA

Katibu Tawala wa Mkoa wa Singida Dkt. Fatma Mganga amewapokea Madaktari Bingwa na Bingwa Bobezi 50 wa Rais Samia , Dkt. Fatma Mganga na kuwataka kuwahudumia Watanzania wa mkoa huo kwa moyo wa upendo na kuacha kumbukumbu hata baada ya kuondoka.

Dkt. Mganga amesema hayo Aprili 28, 2025, wakati wa mapokezi ya madaktari hao watakaofanya kazi za kibingwa na ubingwa bobezi katika halmashauri saba (7) za mkoa huo, sambamba na kuwajengea uwezo watumishi wa afya waliopo katika ngazi za msingi.

"Kambi ya mwaka jana ilifanikiwa kwa kiwango kikubwa, ambapo maelfu ya wananchi walihudumiwa kwa weledi na ufanisi. Mwaka huu tumejipanga kuvuka mafanikio hayo, kwa kutoa huduma bora zaidi na kuwafikia wananchi wengi zaidi," amesema Dkt. Mganga.

"Tunamshukuru Rais Samia kwa maono yake katika kuboresha sekta ya afya. Wananchi tuendelee kuiunga mkono Serikali katika juhudi zake za kutafuta afya bora kwa wote. Pia nawapongeza watumishi wa sekta hii kwa kazi yenu ngumu ya kuwahudumia wananchi," ameongeza Dkt. Mganga.

Dkt. Mganga ametoa wito kwa wananchi kufika hospitalini hapo kupata huduma hizo za kibingwa, akisisitiza kuwa fursa hiyo ni adimu na kwamba madaktari hao wanakuja mara chache, hivyo ni muhimu kuitumia ipasavyo.

Kwa upande wake, Mkuu wa Programu ya Uzazi Salama Wizara ya Afya, Dkt. Phineas Sospeter, amesema kambi hiyo inatoa fursa kwa wananchi, hususan wale wanaoishi katika maeneo ya Singida na mikoa jirani, kupata huduma za kibingwa bila kulazimika kusafiri umbali mrefu.

Dkt. Phineas Sospeter amesisitiza kuwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ameona umuhimu wa kuwafikia wananchi katika ngazi za chini, ambazo mara nyingi hukosa huduma hizo muhimu.

Madaktari Bingwa wa Rais Samia wapo mkoani Singida na watatoa huduma kwenye halmashauri zote kuanzia tarehe 28 Aprili hadi Mei 3, 2025.