MAAMBUKIZI YA VVU YAPUNGUA KWA ASILIMIA 0.7 RUVUMA
Posted on: November 26th, 2024Na WAF - Ruvuma
Imetajwa kuwa maambukizi mapya ya Virusi Vya UKIMWI yamepungua kwa asilimia 0.7 kutoka asilimia 5.6 mwaka 2017 hadi kufikia asilimia 4.9 mwaka 2022.
Hayo yamesemwa leo Novemba 25, 2024 na Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Kanali Ahmed Abbas Ahmed wakati akifungua wiki ya maadhimisho ya siku ya UKIMWI duniani ambayo kitaifa yanafanyika mkoani humo.
Akielezea hali ya maambukizi katika mkoa huo, Kanali Abbas amesema Mkoa wa Ruvuma una jumla ya watu 68,237 wanaoishi na VVU ambapo wanaume ni 24,959 sawa na asilimia 37 na wanawake ni 43,000 sawa na asilimia 63 huku watoto chini ya miaka 15 ni 2382 sawa na asilimia 3.5.
"Halmashauri zinazoongoza ni Manispaa ya Songea ikifuatiwa na Tunduru na Mbinga hivyo nawasihii watu wanao ishi na Virusi vya UKIMWI (WAVIU) wote kuzingatia tiba na matunzo ikiwa ni pamoja na matumizi ya dawa za kufubaza virusi ikiwa ndiyo njia pekee ya kukabiliana na ugonjwa huu," amesema Kanali Abbas.
Aidha, ametaja vichocheo vinavyosababisha maambukizi mapya kuwa ni pamoja na mwingiliano wa watu na shughuli za kiuchumi hivyo amewataka wananchi kujikinga ili wasipate maambukizi.
Naye Mkuu wa Programu kutoka Wizara ya Afya Dkt. Catherine Joachim ameupongeza Mkoa wa Ruvuma kwa mapambano ya kushusha kiwango cha maambukizi ikiwa ni pamoja na kuongoza kwa upimaji wa virusi vya UKIMWI kitaifa.
"Mkoa wa Ruvuma umeendelea kufanya vizuri katika viwango vya “95 95 95” ambapo utafiti wa mwaka 2023 unaonesha asilimia 82 za wananchi wa mkoa huo wanatambua hali zao za maambukizi na asilimia 97 wanatumia dawa za kufubaza virusi vya UKIMWI na asilimia 90 ya wanaotumia dawa wameshafubaza virusi hivyo", ameeleza Dkt. Catherine.
Wiki ya Maadhimisho ya siku ya UKIMWI duniani yanafanyika katika mikoa mbalimbali nchini ambapo kitaifa yanafanyika Mkoani Ruvuma na yanatarajiwa kufungwa tarehe 1 Desemba, 2024 na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Phillip Mpango.