Customer Feedback Centre

Ministry of Health

LITEMBO HOSPITALI YAPATIWA GARI YA WAGONJWA, DAKTARI, MUUGUZI, WATAALAM WA MAABARA

Posted on: April 22nd, 2025

Na WAF - Mbinga, Ruvuma


Katika kutekeleza maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan, Waziri wa Afya Mhe. Jenista Mhagama ametoa gari moja la wagonjwa (ambulance), wataalam wawili wa maabara, daktari mmoja pamoja na muuguzi mmoja ili kupunguza changamoto katika Hospitali ya Litembo. 


 Waziri Mhagama ametekeleza maagizo hayo leo Aprili 22, 2025 na kumuagiza Mwakilishi wa Katibu Mkuu Wizara ya Afya Bw. Danny Temba kupeleka ambulance hiyo kabla ya kurudi Dodoma ikiwa ni katika hatua za kuendelea kuboresha sekta ya afya nchini baada ya kufanya ziara katika Hospitali ya Litembo pamoja na Chuo cha Sayansi Shirikishi Litembo kilichopo katika wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma. 


"Mheshimiwa Rais ameniagiza nitoe gari la wagonjwa lije katika hospitali hii ili kusaidia wagonjwa wa dharura, ameniagiza nilete walimu wawili wenye shahada (Degree) ambao ni wataalam wa maabara wabobezi, mganga (Daktari) pamoja na muuguzi mmoja ili kupunguza changamoto za uhaba huo katika hospitali yetu," amesema Waziri Mhagama. 


"Mhe. Rais Samia baada ya kusikia changamoto hizi, alituelekeza sisi wasaidizi wake kuwaletea gari pamoja na watumishi, kwenye ajira mpya zilizotangazwa kupitia halmashauri ya wilaya ya Mbiga tutaleta daktari mmoja na muuguzi mmoja na mimi nimekuja kutekeleza maelekezo ya Rais sio kutoa ahadi," amesisitiza Waziri Mhagama.


Aidha, Waziri Mhagama amesema Watanzania wana kila sababu ya kumshukuru sana Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa kipaumbele kwenye sekta ya afya kwani amejenga zahanati, Vituo vya Afya vya kisasa nchi nzima pamoja na ukarabati wa hospitali ya wilaya ya Mbinga. 


"Katika uboreshaji huo umewezesha asilimia 75-80 ya wananchi wa Tanzania kuwa na uwezo wa kufika kupata huduma za afya ndani ya kilometa tano (5) kutoka mahala wanapoishi kwa kushirikiana na wenzetu wa sekta binafsi kwakuwa wao ni washirika wa Serikali na sio washindani," amesema Waziri Mhagama. 


Katika hatua nyingine, Waziri Mhagama amewataka wanafunzi wa Chuo cha Afya na Sayansi Shirikishi Litembo, kilichopo Halmashauri ya Mbinga kuzingatia masomo yao kwa kuwa huduma wanazokwenda kuzitoa ni huduma za msingi ambazo Watanzania wanazihitaji tena zikiwa sahihi na zenye ubora. 


"Nawaomba sana mzingatie yale ambayo mnayasoma kwa kuwa kwenye sekta ya afya upande wa tiba, chochote ambacho utakifanya kwa makosa madhara yake ni makubwa ikiwemo kusababisha kifo kwa mgonjwa, naomba mjifunze kwa bidii, mjifunze kwa kuelewa ili mkawe wataalam bora kwa jamii na tupunguze changamoto za watumishi nchini," amesema Waziri Mhagama.  


Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Nyasa Mhe. Peres Magiri akimuwakilisha Mkuu wa Wilaya ya Mbinga Mhe. Kisare Magori amesema wataendelea kusimamia masuala yoye ya kiutendaji kwa kufanya kazi kwa weledi. 


"Kwa niaba ya Serikali ya Wilaya ya Mbinga, sisi kama viongozi tumepokea maelekezo yako Mhe. Waziri na kuyatekeleza kwa haraka iwezekanavyo ili wananchi wapate huduma bora na kuendeleza juhudi za Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan za kuboresha sekta ya afya nchini," amesema Mhe. Magiri