Customer Feedback Centre

Ministry of Health

KWA PAMOJA TUZUIE VITENDO VYA UKATILI WA KIJINSIA - WAZIRI UMMY

Posted on: November 30th, 2023

Na. WAF - Tanga 


Watanzania wametakiwa kushirikiana kwa pamoja kupambana kwa kuzuia vitendo vya ukatili wa kijinsia ikiwemo kuzuia suala la mimba za utotoni kwa kuwaacha watoto wa kike wasome na watimize ndoto zao. 


Waziri wa Afya Mhe. Ummy Mwalimu amesema hayo leo Novemba 30, 2023 kwenye kilele cha Maadhimisho ya siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia yaliyofanyika Wilaya ya Muheza Mkoani Tanga ambapo amesema kuwa mimba za utotoni ni asilimia 22, yaani katika kila watoto wa kike 100, watoto 22 wanapata ujauzito katika umri mdogo. 


Aidha, Waziri Ummy amewataka madaktari wote nchini kuacha kuogopa kutoa taarifa sahihi za vitendo vya ukatili, kama mtoto amebakwa sema na kama mtoto ameingiliwa kinyume na maumbile sema kwa kuwa hatovumiliwa mtu yeyote atakaeficha ukweli kuhusu vitendo vya kikatili.


“Serikali haitomvumilia mtu yoyote wa ubakaji na walawiti wa watoto, madaktari nawasisitiza msiogope kutoa taarifa sahihi kuna baadhi wanaogopa kutoa taarifa za kweli, msiogope, polisi kazi yao ni kutafuta ushahidi Sasa mnapoogopa kutoa ushahidi mnachangia kuendeleza ukatili wa kijinsia kwa watoto.” Amesema Waziri Ummy 


Pia, amesisitiza kwa Wakuu wa Wilaya na Mikoa nchini kuzingatia maelekezo ya Serikali ikiwemo kuhakikisha kila shule ya Msingi na Sekondari inakuwa na walimu malezi ambao watakuwa ndio kimbilio la watoto kueleza matatizo ya ukatili wanayofanyiwa wakiwa shule au nyumbani. 


Waziri Ummy akiendelea kutoa athari za vitendo vya ukatili wa kijinsia amesema Tanzania inatumia asilimia 3.5 ya Pato la Taifa kwa ajili ya kushuhulikia masuala ya ukatili wa kijinsia ambapo fedha hizo zingeweza kutumika kwenye masuala ya Afya, kwenye maji lakini pia kwenye masuala ya elimu kwa watoto. 


Waziri Ummy amewahakikishia Watanzania kuwa Serikali chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan itaendelea kusimamia utekelezaji wa sheria ili kupambana na vitendo vya ukatili wa kijinsia hususani kwa wanawake na watoto. 


Kwa upande wake Balozi wa Ireland nchini Tanzania Mhe. Mary Oj’Neill ameipongeza Tanzania na kuahidi kuendelea kuunga mkono jitihada za Tanzania katika kutokomeza vitendo vya ukatili wa kijinsia. 


Maadhimisho haya yaliyoandaliwa na Mkoa wa Tanga kwa kushirikiana na Wadau wa Maendeleo wakiwemo Shirika la Femina Hip, UZIKWASA pamoja na Ubalozi wa Ireland nchini Tanzania. 


Lengo la Maadhimisho hayo ya siku 16 za Kupinga ukatili wa kijinsia ni kutumia siku hizi kwa kutoa elimu, hamasa, taarifa pamoja na kupanga mikakati kwa ajili ya kutokomeza vitendo vya ukatili wa kijinsia.


Kauli mbiu ya Maadhimisho hayo kwa Mwaka huu inasema ‘wekeza kuzuia ukatili wa kijinsia’