Customer Feedback Centre

Ministry of Health

KAYA YA WATU SITA WATAJIUNGA NA BIMA YA AFYA KWA WOTE KWA 340,000/= KWA MWAKA

Posted on: October 7th, 2022

Na. WAF - Dodoma

Kiwango cha kujiunga na Bima ya Afya kwa wote ni Shilingi 340,000 kwa kaya ya watu Sita akiwemo mchangiaji, mwenza wake na wategemezi wasiozidi wanne kwa mwaka pindi sheria hiyo itakapojadiliwa na kupitishwa na bunge.

Hayo yamesemwa na Katibu Mkuu Wizara ya Afya Prof. Abel Makubi leo wakati wa kikao na Wakurugenzi wa Wizara na Taasisi zilizo chini ya Wizara ya Afya kuhusu Sheria ya Bima ya Afya kwa wote kilichofanyika katika Hospitali ya Benjamin Mkapa Jijini Dodoma.

Prof. Makubi amesema wale ambao hawana familia watachangia kiasi cha shilingi 84,000 kwa mtu mmoja mmoja kwa mwaka ambayo ni sawa na wastani wa shilingi 7,000 kwa mwezi.

Prof. Makubi amebainisha kuwa kwa wananchi watakaotambuliwa kutokuwa na uwezo wataendelea kupatiwa huduma kwa utaratibu utakaowekwa na Serikali kwa kila mtu kuwa na kadi yake ya Bima ya Afya.

"TASAF na mifumo ya maendeleo ya jamii ndio itakayofanya utambuzi kwa wananchi wasio na uwezo ili kuiwezesha Serikali kuweka utaratibu madhubuti wa kutoa huduma kwa wananchi wasio na uwezo kupata huduma pindi wanapohitaji". Amesema Prof. Makubi.

Aidha, Prof. Makubi ameweka wazi kuwa endapo sheria itapitishwa basi Wizara imejipanga kuanza mara moja utekelezaji wa sheria hii bila kikwazo ifikapo Julai 1, 2023 kwani suala hilo sio la ghafla.

"Suala la sheria ya bima ya afya kwa wote sio dharura limefanyiwa mchakato kwa muda mrefu zaidi ya miaka 10 kwa ushirikishi mkubwa wa wadau." Amesema Prof. Makubi

Muswada wa sheria hiyo ulisomwa kwa mara ya kwanza katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Septemba 27, 2022.

Katika kuonesha umuhimu wa kutungwa kwa Sheria ya Bima ya Afya kwa wote Prof. Makubi amesema kutawezesha wananchi wengi kuwa katika mfumo wa Bima ya Afya na hivyo kuwa na uhakika wa kupata huduma za Afya pindi mwananchi anapohitaji.

Mwisho, ametoa rai kwa watoa huduma kupitia Bima ya Afya kupunguza mlolongo mrefu wa utoaji wa huduma kwa mteja kuanzia anapoingia getini hadi anapotoka ili kuokoa muda wa mteja kwa kupata huduma kwa wakati.