KATAVI RRH YAMKOSHA RAIS SAMIA KWA USAFI
Posted on: July 14th, 2024
Na. Majid Abdulkarim, Katavi
Rais wa Jamahuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amepongeza utendaji kazi wa Menejimeti ya Hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Katavi kwa usafi uliopo Hospitalini hapo.
Akizungumza leo Julai 14,2024 wakati wa ziara yake ya ukaguzi wa Hospitali hiyo, Rais Samia amesema alichokiona katika Hospitali hiyo ni suala la kupigiwa mfano kwa hospitali zingine nchini
"Ndugu zangu nimesimama kuelezea furaha yangu nimefika kukagua Hospitali na kuona inavyoendelea starehe yangu ni nilichokiona hapa ndani hakina tofauti na kilichopo kwenye Hospitali ni kubwa ambao nao kwa sasa wamejidhatiti juu ya suala la usafi muendele hivi hata kama ujenzi bado una unaendelea,"amesema Rais Samia.
Amesema alipofika eneo hilo hakusikia harufu ya dawa hivyo amempongeza Mganga Mfawidhi wa Hospitali hiyo Dkt. Serafin Patrice na Menejimenti yote ya Hospitali.
"Hospitali hii imenipa faraja wakati naongozwa kuangalia madaktari wote niliofuatana nao ni vijana ambao wangependa kuhudumu kwenye Miji mkubwa kama Dar es Salaam, Arusha au Mwanza lakini vijana wazalendo wamekubali kukaa Katavi na kuhudumia wananchi hongereni sana,"amepongeza Rais Samia.
Kuhusu fedha za ujenzi awamu ya pili, Rais Samia amesema zimefika na Hospitali hiyo itaendelea kujengwa majengo mengine zaidi ili kuhakikisha wananchi wa Katavi na mikoa ya jirani wananufaika na uwekezaji mkubwa wa serikali yao.
Rais Samia amesema Serikali ya awamu ya sita itaendelea kuzisogeza huduma za afya karibu na wananchi na utoaji wa huduma bora.
Amesema fedha zinazotumika kununua vifaa tiba ni nyingi ambapo lengo la Serikali kuhakikisha huduma bora za matibabu zinapatikana mpaka katika ngazi ya msingi mpaka Taifa .
Mwisho