KAMBI YA MADAKTARI BINGWA NZEGA, KIMBILIO LA WAGONJWA WA MASIKIO, PUA NA KOO.
Posted on: May 2nd, 2025
Na WAF, Nzega
Wananchi wanaosumbuliwa na magonjwa kwenye sikio, pua na koo (ENT) wameongoza kwa idadi ya watu waliojitokeza katika kambi ya madaktari bingwa wa Rais Samia katika wilaya ya Nzega, mkoani Tabora.
Hali hiyo imebainika kwenye kambi inayoendelea wiki hii katika Mkoa wa Tabora kwa wilaya zote nane (8) za mkoa huo ambapo hadi kufikia Mei Mosi, 2025 zaidi ya wananchi 500 wamefika katika Hospitali ya Wilaya ya Nzega kwa ajili ya kupata huduma za matibabu ya kibingwa, kati ya hao 60 wakiwa na changamoto ya kiafya kwenye masikio, pua au koo.
Akizungumza wakati huduma za matibabu zikiwa zinaendelea katika kambi hiyo, Mganga Mkuu wa Wilaya ya Nzega Dkt. Anna Chadua, amesema kwenye ukanda wao wamekuwa wakipokea watu wazima na watoto ambao wanasumbuliwa na tatizo hilo.
"Kabla ya ujio wa madaktari hawa, wananchi walikuwa wakihudhuria kati ya 200 hadi 250 lakini ujio huo umewezesha watu wengi kujitokeza kati ya hizi siku tatu hadi watu 500 ambalo ni ongezeko mara mbili," amesema Dkt. Chadua.
Dkt. Chadua ameongeza kuwa walipoona uhitajiwa wa mtaalam wa tiba ya masikio, pua na koo waliwasilisha maombi kwa Wizara na wameshukuru kwa ujio wa wataalam hao katika wilaya ya Nzega.
Katika hatua nyingine wataalam wa Hospitali hiyo, wamewashukuru Madaktari Bingwa wa Mhe. Rais Samia kwa kuwajengea uwezo kwa vitendo.
"Suala la elimu ni endelevu hivyo wanapokuja mabingwa inakuwa ni fursa kwao kujifunza kutokana na maarifa bobezi lakini pia matumizi ya vifaa vya kisasa,” amesema Muuguzi Namaiya Hassan wa Hospitali hiyo.
Naye Dkt. Adela Pontian, Daktari Bingwa wa Magonjwa ya ndani kutoka Hospitali ya Chamwino, amesema wanafurahia kambi hizo kwani wanakutana na madaktari bingwa wengine hali inayo wasaidia kubadilishana uzoefu wa kibingwa.
Madaktari Bingwa wa Rais Samia Suluhu Hassan wameweka kambi katika mkoa wa Tabora kuanzia Aprili 28 hadi Mei 3, 2025 ikiwa ni njia ya kusogeza huduma za kibingwa karibu na wananchi.