Customer Feedback Centre

Ministry of Health

JITIHADA ZA RAIS SAMIA ZASAIDIA KUPUNGUZA VIFO VITOKANAVYO NA UZAZI

Posted on: October 28th, 2023


Na WAF Dar Es Salaam.

 

Jitihada za Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan za kuboresha huduma bora za afya zimesaidia katika kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi kutoka vifo 530 kwa kila vizazi hai 100,000 mwaka 2015/16 na kupungua hadi kufikia vifo 104 kwa kila vizazi hai 100,000 mwaka 2022.

 

Rais Samia amesema hayo leo alipokuwa akizindua ripoti ya tafiti ya afya ya uzazi na mtoto na viashiria vya malaria ya Mwaka 2022 halfa iliyofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere.

 

“Hii ni hatua kubwa, kiwango hiki kimepungua kwa asilimia 80, Mwenyezi Mungu atuwezeshe tuendelee kupunguza na tunaona jitihada zinazofanywa kwenye Sekta ya Afya zinaleta matokeo chanya” Amesema Rais Dkt. Samia.

 

Amesema kuwa kuzaa salama ni baraka ya Mwenyezi Mungu hata hivyo Serikali ina wajibu wa kujipanga kutoa huduma bora za afya kwa wananchi na kuwekeza zaidi kwenye upatikanaji wa vifaa ili wananachi waweze kutoa huduma bora. 

 

“Shabaha ya malengo endelevu ya dunia ya mwaka 2030 inaelekeza kupunguza vifo vya wamama wakati wa uzazi na visizidi 70 kwa kila vizazi hai 100,000, sasa hivi tupo 10, safari yetu mpaka mwaka 2030 tunaweza kufikia hii shabaha”. Amesema Rais Dkt. Samia.

 

Mwelekeo wetu ni mzuri, ndugu zangu madaktari, wauguzi na wakunga tusibweteke twendeni tukaze mwendo vifaa vipo twendeni tukafanye kazi kuokoa uhai wa wenzetu.

 

Kuhusu vifo vya Watoto walio chini ya umri wa miaka 5, Rais Samia amesema kuwa vifo vya Watoto hao vimepungua kutoka 67 kwa kila vizazi hai 100,000 mwaka 2015/16 hadi kufikia vifo 43 kwa kila vizazi hai 100,000.

 

Rais Samia amewataka watendaji na wadau wa Sekta ya Afya kuongeza kasi ya uwajibikaji na kupunguza vifo vya Watoto wachanga ambavyoa amesema kuwa ripoti inaonyesha vifo hivyo vimepungua kwa asilimia 1.

 

Ikumbukwe kuwa mnamo mwaka 2018 akiwa Makamu wa Rais wakati huo Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan alizindua kampeni ya Jiongeze Tuwavushe Salama iliyolenga kuhimiza uwajibikaji wa viongozi na watendaji ndani ya Sekta ya Afya kushughulikia changamoto za Afya ya Uzazi, Mama na Mtoto ili kuweza kufikia malengo endelevu ya 2030 pamoja na kupunguza kwa kiasi kikubwa changamoto za afya ya uzazi.