JENGENI USHIRIKIANO WA UTOAJI HUDUMA BORA ZA AFYA
Posted on: February 7th, 2025
Na WAF, Dodoma
Waziri wa Afya Mhe. Jenista Mhagama amewataka wataalam pamoja na wadau wa Sekta ya Afya kushirikiana katika kuanzisha kituo cha ubunifu wa utoaji wa huduma bora za afya ya mama na mtoto nchini.
Waziri Mhagama ametoa maagizo hayo Februari 06, 2025 alipokutana na wawakishi kutoka katika Hospitali ya Kilutheri ya Haydom, Manyara na kujadiliana kuhusu ushirikiano zaidi wa utoaji wa huduma za afya ya uzazi, mama na mtoto.
“Upo umuhimu wa kuanzisha kituo cha umahiri wa utoaji wa huduma bora za afya ya uzazi mama na mtoto, tunataka kuwa na kituo ambacho kitatoa fursa kwa wataalam kubuni njia bora za kuboresha huduma za afya ya uzazi ikiwa ni pamoja na matumizi ya teknolojia za kisasa za kufuatilia afya ya mama na mtoto,” amefafanua Waziri Mhagama.
Amesema kituo hicho pia kitakuwa jukwaa la kuanzisha miradi ya elimu kuhusu lishe bora, huduma za uzazi, na uangalizi wa watoto wachanga ambapo lengo kuu likiwa ni kuhakikisha kuwa huduma hizi zinapatikana kwa urahisi na zenye ubora kwa familia katika maeneo yote nchini.
Waziri Mhagama amesema kuwa Serikali imepiga hatua katika kupunguza vifo vya mama na mtoto kwa kuanzisha mikakati madhubuti ya kuboresha huduma za afya katika ngazi zote ikiwemo uwekezaji katika miundombinu ya afya, upatikanaji wa huduma za uzazi pamoja na mafunzo kwa wahudumu wa afya.
Hata hivyo amesema bado mbinu mpya pamoja na mikakati endelevu ya uboreshaji huduma za afya ya uzazi zinahitajika zaidi ili kuboresha huduma za afya ya uzazi, mama na mtoto.
Kwa upande wake Dkt. Paschal Mdoe kutoka Hospitali ya Haydom amesema wataendelea kushirikiana na Serikali katika utoaji wa huduma bora za afya ikiwemo masuala ya afya ya uzazi mama na mtoto ili wananchi waendelee kupata huduma bora.
Dkt. Mdoe amesema kuwa katika Hospitali ya Haydom wamebuni kitita cha uzazi salama ambapo malengo ya kuanzisha kitita hicho ni kuhakikisha uwepo wa huduma bora za uzazi zinazolingana na vipaumbele vya Wizara ya Afya, na hatimaye kupunguza vifo vya akina mama na watoto wachanga wakati na baada ya kujifungua.