Customer Feedback Centre

Ministry of Health

HUDUMA ZA UKUNGA NYENZO MUHIMU KATIKA UTOAJI WA HUDUMA ZA AFYA NCHINI

Posted on: May 6th, 2025

Na WAF - SHINYANGA

Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Anamringi Macha amesema wakunga ni nyenzo muhimu katika utoaji wa huduma za afya chini kwani huduma wanazotoa ni muhimu katika kuokoa maisha, afya ya familia na kuimarisha ustawi wa jamii kwa ujumla.

Mhe. Macha ameyasema hayo Leo tarehe 05 Mei, 2025 katika kilele cha maadhimisho ya siku ya Mkunga Duniani yaliyo fanyika Mkoani Shinyanga.

Mkuu huyo wa Mkoa ameongeza kuwa zaidi ya Asilimia 60 ya watumishi katika sekta ya afya ni wauuguzi na wakunga hivyo ni muhimu kuthamini mchango wao katika utoaji wa huduma kwa wananchi.

Mhe. Macha amesema Serikali ya Awamu ya Sita imeboresha huduma kwa kujenga na kukarabati majengo, pamoja na nyumba za watumishi ili huduma zipatikane wakati wote akizitaja juhudi hizi kupunguza vifo vya mama na mtoto kwa kiwango kinachoonekana mara moja tu katika vizazi hai laki moja.

Aidha ameongeza kuwa Serikali inaendelea kuajiri wahudumu wa afya, wakiwemo wakunga, ili kuongeza upatikanaji wa huduma bora kwa wananchi lakini pia Uajiri huu umeondoa uhaba wa watumishi katika maeneo ya mbali, hivyo kuboresha huduma za afya kwa mama na mtoto, na kupunguza vifo vinavyotokana na uzazi.

Aidha, Mhe. Macha amesema maboresho hayo yamezingatia sana sehemu za kutolea huduma za mama na mtoto na kuhakikisha kuwa wodi za watoto wachanga na wale wenye matatizo zinajengwa kwenye hospitali za Mikoa,Wilaya na baadhi ya vituo vya afya.

Kwa upande wake Mkurugenzi msaidizi wa usimamizi wa ubora wa huduma za uuguzi na ukunga Wizara ya Afya, Saturini Manangwa amesema wakunga wana uwezo wa kutoa huduma za afya kwa zaidi ya asilimia 90 huku akisema utafiti unaonyesha endapo huduma za ukunga zitatolewa kwa ukamilifu zitapunguza vifo Vitokanavyo na uzazi.

Manangwa ameitimisha kuwa tuendelee kushirikiana kwa pamoja ili kuhakikisha hakuna vifo vinatokea kwa sababu ya huduma zinazotolewa na wakunga.