Customer Feedback Centre

Ministry of Health

HUDUMA ZA UCHUNGUZI NGUZO KUU YA SEKTA YA AFYA NCHINI

Posted on: October 3rd, 2025

Na. WAF, Dar es Salaam

Huduma za uchunguzi na maabara zimekuwa miongoni mwa nguzo kuu na zenye mchango mkubwa katika kuboresha utoaji wa huduma bora za afya nchini.

Hayo yamesemwa na Mganga Mkuu wa Serikali, Dkt. Grace Magembe, Oktoba 02, 2025 katika Ukumbi wa Mikutano wa Mwalimu Julius Nyerere jijini Dar es Salaam katika Mkutano wa Afya wa Tanzania (THS) unaoendelea jijini humo.

Dkt. Magembe amesema ni ukweli usiopingika kwamba huduma za maabara ndio uti wa mgongo wa huduma zote za matibabu ikiwemo huduma za kinga, tiba na huduma za uchunguzi katika vituo vya kutolea huduma za afya kuanzia ngazi ya msingi hadi taifa.

“Eneo hili la maabara limekuwa karibu sana na moyo wangu na ni moja wapo ya kazi muhimu ndani ya sekta ya afya katika utoaji wa huduma kwani bila maabara na huduma bora za uchunguzi basi hakuna sekta ya afya,” amesema Dkt. Magembe.

Pia, Dkt. Magembe amesema huduma za maabara haziishii kwenye magonjwa ya kuambukiza pekee, bali hata magonjwa yasiyo ya kuambukiza sasa yanaonesha umuhimu wa uchunguzi wa maabara katika usimamizi wa magonjwa, ambayo ni tishio kubwa kwa mfumo wa afya.

“Tumekuwa na uzoefu huko nyuma, na hata sasa, wakati wa milipuko, wakati wa janga la UVIKO-19, kwangu mimi huduma za maabara zinaenda mbali zaidi ya kusaidia utambuzi au kuzuia magonjwa ya kuambukiza pekee, bali hata kwa magonjwa yasiyoambukiza,” amesema Dkt. Magembe.

Aidha, amesema Serikali kupitia sekta ya afya inatarajia ifikapo 2030 kuwa na maabara za mikoa na taifa zenye usajili wa kimataifa na maabara za ngazi ya wilaya kufikia kiwango cha nyota tatu cha Shirika la Afya Duniani (WHO).